Home Uchumi Mazingira WATAALAMU WAGUNDUA MTI WA MIAKA 3,000 KATIKA MISITU YA UDZUNGWA.

WATAALAMU WAGUNDUA MTI WA MIAKA 3,000 KATIKA MISITU YA UDZUNGWA.

34
1

Na Hafsa Omar.

Wataalamu wa utafiti wa mazingira nchini Tanzania wamegundua mti wa kipekee unaokadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 3,000 katika Misitu ya Milima ya Udzungwa, hatua inayotajwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika historia ya tafiti za misitu ya tropiki duniani.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa mwaka 2025 katika Jarida la kitaalamu la Phytotaxa, timu ya wanasayansi wa ndani na kimataifa ilifanya uchunguzi wa kina kwa kutumia mbinu za kisasa za kupima mzunguko wa ukuaji wa miti (annual growth rings), na matokeo yake yakabaini kwamba baadhi ya miti katika eneo hilo inaishi kwa maelfu ya miaka  jambo ambalo halikuwahi kudhaniwa katika mazingira ya tropiki kama Udzungwa.

“Tulishangazwa na matokeo tuliyoyapata. Kwa muda mrefu tuliamini kuwa miti ya kitropiki haiwezi kufikia umri mkubwa kutokana na mzunguko wa mvua mara mbili kwa mwaka na hali ya kuoza kwa kasi. Lakini mti huu ni ushahidi hai kwamba mazingira yanapodumishwa, maisha ya asili yanaweza kudumu kwa milenia,” alisema mmoja wa watafiti wakuu wa mradi huo.

Taarifa zaidi kutoka Mongabay, tovuti ya kimataifa ya mazingira, zinaeleza kuwa urefu na ukubwa wa mizizi ya mti huo umebadilisha mwelekeo wa tafiti za mimea duniani ambapo Uwezo wake wa kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa kwa muda mrefu unadhihirisha jinsi spishi za asili zinavyoweza kuhimili vikwazo vya kiasili endapo mazingira yanahifadhiwa ipasavyo.

kwa mujibu wa aataalamu hao wanasema spishi hiyo adimu inapatikana katika maeneo machache tu yenye ulinzi maalum ndani ya Udzungwa, na kwamba idadi yake ni ndogo sana. Kwa sababu hiyo, ipo katika hatari kubwa ya kutoweka endapo hifadhi hizo zitaharibiwa kwa moto, ukataji miti au shughuli za kibinadamu.

“Ugunduzi huu si tu unaongeza maarifa kuhusu misitu ya tropiki, bali pia ni onyo kwetu kulinda zaidi mazingira yetu. Kila mti wa aina hii ni kama jalada la historia ya dunia, linatupa hadithi ya mabadiliko ya tabianchi kwa maelfu ya miaka,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa sasa, timu ya watafiti inaendelea na uchunguzi wa kina kutambua idadi kamili ya miti ya aina hiyo na kuchunguza uwezekano wa kuwepo kwa spishi nyingine zenye umri unaofanana katika milima mingine ya misitu nchini.

1 COMMENT

Leave a Reply to jina Cancel reply

Please enter your comment!
Please enter your name here