Na Said Khamis.14/11/2025
Wakulima wa zao la mwani katika kijiji cha Paje wamesema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa chanzo kikuu cha kuathiri uzalishaji wa mwani, hasa katika vipindi vya joto kali vinavyosababisha zao hilo kuharibika kabla ya kuvunwa. Wamesema kwamba ongezeko la joto na kubadilika kwa misimu ya mvua kumeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wao wa kuzalisha mwani kwa ubora unaohitajika sokoni.
Wakizungumza na TOZ, wakulima hao wamesema kuwa katika kipindi cha miezi ya joto, mwani hukosa uimara na kubadilika rangi, hali inayosababisha zao hilo kuoza kabla ya kuvunwa ambapo wameeleza hali hiyo imekuwa ikipunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji na kuwanyima kipato walichokitarajia kupata kupitia kilimo hicho ambacho kimekuwa tegemeo kuu kwa familia nyingi katika kijiji hicho.

“Tunaathirika sana tukipata joto kali kama hili. Mara nyingi tunakuwa tumeshatumia nguvu na muda mwingi kupanda mwani, lakini unaharibika kabla hatujauvuna. Hii inaumiza sana kwa sababu ndiyo tunategemea kujikimu,” wamesema baadhi ya wakulima hao.
Aidha, wametaka kuongezewa mafunzo ya mbinu bora za kilimo cha mwani ili kuzalisha kwa tija zaidi na kuweza kukabiliana na athari zinazoletwa na mazingira yanayobadilika. Wameeleza kuwa bila kupata ujuzi zaidi na usaidizi wa kitaalamu, uzalishaji wao unaweza kuendelea kushuka mwaka hadi mwaka
Sambamba na hayo wakulima hao waliiomba Idara ya maendeleo ya uvuvi na mazao ya baharini kuendelea kuwapatia mafunzo ya kudhibiti na kutunza zao la mwani ili kwenda sambamba na madadiliko ya tabia ya nchi.
Mbali na athari za kimazingira, wakulima hao wametoa wito kwa serikali na wadau wa sekta ya bahari kuongeza bei ya mwani ili kuendana na gharama wanazopata wakati wa uzalishaji. Wamesema kuwa ongezeko la bei litawasaidia kukabiliana na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwapa uwezo wa kuendelea na shughuli za uzalishaji bila kupata hasara kubwa.
Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya uvuvi na mazao ya baharini Dk Salum Sudi Hamed, amewataka Wakuilima wa zao hilo kulima katika kina kirefu cha maji ili kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi. wakati akizungumza na TOZ huko Maruhubi, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharib.

Dk Salum alisema ongezeko la joto huathiri ubora wa mwani kutokana na kushindwa kuzalisha virutubisho vya kutosha na kupelekea mwani huo kuharibika.
Ameeleza kuwa athari hiyo ilionekana zaidi katika maeneo ya kijiji cha Paje, Bwejuu na Jambiani ambayo yalikuwa yakilima mwani kwa wingi, hivyo kutokana na ongezeko la joto ni lazima wakulima wa zao hilo kulima mwani katika kina kirefu cha maji.

Mkurugenzi huyo aliongeza kusema kuwa kubadilika kwa miongo hupelekea kubadilika kwa vitu vingi ikiwemo uzalishaji wa mwani.
‘’Kipindi tunachotegemea kupata mvua nyingi unakuta tunapata mvua kidogo kuliko mwaka uliopita na kipindi tunachotegea kupata mvua kidogo tunapata mvua nyingi kuliko kawaida na hata hali ya jua huathiri zao hilo’’ amesema dk Salum.
Zanzibar ni miongoni mwa nchi za visiwa zinazokabiliwa na athari mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuongezeka kwa joto kali ambalo limekuwa likiathiri shughuli nyingi za uzalishaji.






















mabqadiliko ni hatari sana, kila kitu kimeharibika