Na Said Khamis, 15/11/2025.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia ipasavyo haki na fursa za watu wenye ulemavu, sambamba na kuimarisha miundombinu na huduma muhimu zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Hayo yalielezwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, wakati akisoma hutuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, huko Katika ukumbi wa Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Katibu huyo alisema, serikali imeweka mkazo kuhakikisha kundi hilo linapata huduma stahiki kama ilivyoelekezwa katika sheria ya watu wenye ulemavu Na. 8 ya mwaka 2022.

Alieleza kuwa sheria hiyo imeweka misingi imara ya kuwalinda na kuwaendeleza watu wenye ulemavu pamoja na kuanzisha mabaraza ya Wilaya ya watu wenye ulemavu kwa lengo la kuhakikisha wanatambulika na kujumuishwa katika sera, sheria, mipango na programu mbali mbali za maendeleo.
“Serikali inatoa msisitizo kuhakikisha haki na fursa za watu wenye ulemavu zinaendelea kusimamiwa vizuri Zanzibar. Hili ni jukumu letu na ni sehemu ya utekelezaji wa sheria,” alisema Ussi.
Aliongeza kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua mbali mbali za kuhakikisha watu wenye Ulemavu wanapata fursa sawa kama walivyo watu wengine.
Alisema ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki ya msingi ya elimu, serikali imejenga skuli mbili za dakhalia za watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata elimu bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti kutoka Jumuiya ya wasioona Zanzibar (ZANAB) Fatma Djaa Shesa alisema , chanzo cha matumizi ya fimbo nyeupe kimetokea mwaka 1922, ambapo mtu wa kwanza kuitumia alikuwa James William, mpiga picha na mwandishi wa habari kutoka Uingereza.
Fatma alisema historia hiyo inaendelea kuwa msingi muhimu katika kutambua haki na uhuru wa watu wasioona duniani.
Aidha, alisema kwa miaka mingi walitegemea kusafirishwa kwenda bara ili kushiriki maadhimisho hayo lakini sasa Zanzibar imeanza kuadhimisha siku hiyo.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imeongeza uelewa, hamasa na kujenga utambulisho wao kama watu wenye ulemavu wa kuona ndani ya nchi.
Naye Mwenyekiti Wa Shirikishiko la Jumuiya za Watu Wenye ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) Mwandawa Khamis Mohammed, alisema maadhisho hayo yanatoa mwamko mpya kwa jamii kuhusu matumizi ya fimbo hiyo, kwani wengi nje ya maeneo rasmi hawakuwa na uelewa wake.

Akitoa neno la shukrani katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa ZANAB Muhammed Salum Mabrouk aliishukuru serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu na kusema hatua za kuimarisha elimu, afya na miundombinu zinaonyesha dhati ya serikali katika kuhakikisha haki zao zinaendelezwa kikamilifu.
Maadhimisho ya siku ya fimbo nyeupe duniani yameadhimishwa Zanzibar kwa mara ya kwanza, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Uwezeshaji na Uimarishaji wa watu wasioona Zanzibar ni haki yetu sote”





















