Home Siasa ZAMECO YAPINGA KUDHIBITI VYOMBO VYA HABARI, YATETEA UHURU WA TAARIFA KIPINDI CHA...

ZAMECO YAPINGA KUDHIBITI VYOMBO VYA HABARI, YATETEA UHURU WA TAARIFA KIPINDI CHA UCHAGUZI.

30
0

Na Fatma Rajab.

Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imepinga vikali uamuzi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar kutangaza orodha ya vyombo vya habari vya mtandaoni vinavyodaiwa kufanya kazi kinyume cha sheria, ikisema hatua hiyo inatishia uhuru wa habari na haki ya wananchi kupata taarifa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa tarehe 25 Oktoba 2025, ZAMECO imesema hatua ya kutaja hadharani majina ya televisheni za mtandaoni kama Tifu Online TV, Marhaba Online TV, Vuga Online TV, Busati Online TV, Kasusi Online TV, Digital Online TV, Leaders Online TV, Zanzibar Yetu Online TV, Mawengi Online TV, Jimbi Online TV na Mu Online TV bila kujumuisha wadau ni kinyume na misingi ya ushirikishwaji na uwazi.

“Kitendo cha Tume kuvitaja vyombo hivyo hadharani bila ya kuhusisha majadiliano jumuishi na wadau kinadhihirisha nia ya kuzuia uhuru wa kujieleza na haki ya watu kupata taarifa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

ZAMECO imesisitiza kuwa haki ya kupata taarifa ni ya kikatiba kama inavyobainishwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (toleo la 2010) na mikataba ya kimataifa kama Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR) na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR).

Aidha Kwa mujibu wa ZAMECO, vyombo vya habari vya mtandaoni si tu vimechangia kukuza demokrasia na utoaji wa taarifa huru, bali pia vimekuwa chanzo cha ajira kwa vijana wengi wanaojiajiri kupitia teknolojia. “Kuwepo kwa mitandao hiyo kumewawezesha vijana kujipatia kipato na wengine kutumia majukwaa hayo kama sehemu ya mafunzo yao ya vitendo waliyopata vyuoni,” wamesema.

ZAMECO imetoa mfano wa Afrika Kusini, ambapo Media Development and Diversity Agency Act, 2002 imeweka mfumo wa kusaidia vyombo vya habari kupitia ruzuku, mafunzo, na msaada wa kiufundi badala ya kuvifungia. Wamesisitiza kuwa Tume ya Utangazaji Zanzibar inapaswa kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari badala ya kutumia mbinu za vikwazo.

“Ni muhimu kuzingatia kuwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, kila sauti na jukwaa la habari lina nafasi kubwa katika kukuza amani, mshikamano na maamuzi yenye ufahamu miongoni mwa wananchi,” imeongeza taarifa hiyo.

Aidha, ZAMECO imelaani tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali kunyima ushirikiano kwa waandishi wa habari, hasa vijana, katika kutafuta taarifa, ikisema hali hiyo inavunja moyo waandishi na kudhoofisha juhudi za kuimarisha uwajibikaji serikalini.

Taarifa hiyo imetolewa kwa pamoja na wadau wa habari wakiwemo Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Baraza la Habari Tanzania Zanzibar (MCT-ZNZ), na Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Zanzibar (THRDC-ZNZ).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here