Na Said Khamis, 15/11/2025.
Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu zote mbili (elimu ya sekula na elimu ya madrasa) ili kuwajengea mafanikio ya dunia na Akhera.
Wito huo umetolewa na Mshauri wa Masuala ya Kiislam Zanzibar, Sheikh Ahmed Haidar Al-Farsiy, katika hafla ya Siku ya Wazazi iliyofanyika katika Skuli ya Asco Muslim, Kianga, Wilaya ya Magharibi A.
Sheikh Haidar alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapeleka watoto wao kwenye elimu ya sekula pekee, jambo ambalo linakwenda kinyume na maelekezo ya Allah S.W. Alisisitiza kuwa mzazi au mlezi anayehakikisha mtoto wake anasoma elimu ya dini ya Kiislam atapata malipo makubwa duniani na Akhera.
“Sijambo baya kwa Muislam kusoma elimu ya dunia. Tunahitaji madaktari, wakunga na wataalamu wengine. Lakini elimu ya Akhera pia ni lazima, ili tupate Masheikh, Maulamaa, Maimamu na walimu wa madrasa,” alisema Sheikh Haidar.

Aidha, alizungumzia umuhimu wa jamii ya Kiislam kutambua thamani ya dini yao ili waweze kulea watoto katika misingi ya maadili mema kwa ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa skuli hiyo, Sheikh Ali Saleh Kombo, alisema Skuli ya Asco Muslim imefanikiwa kwa mara ya kwanza kuanzisha madarasa ya tatu na nne tangu kuanzishwa kwake. Alibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha elimu ya dini ya Kiislam inaingizwa katika sekta zote, ikiwemo skuli za kawaida.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa moja ya mafanikio makubwa ya skuli hiyo ni kuwahifadhisha Qur’ani wanafunzi, jambo ambalo ni miongoni mwa malengo ya msingi ya taasisi hiyo.
“Tunataka skuli yetu itambulike kitaifa na kimataifa kwa kutoa wanafunzi waliokamilisha kuhifadhi Juzuu 30,” alisema.

Katika risala iliyosomwa na mwanafunzi wa skuli hiyo, Maitham Abdul Rahman Ali, ilielezwa kuwa dhamira ya skuli ni kuwa moja ya skuli kubwa za Kiislam Zanzibar na Tanzania, ikitoa taaluma mbalimbali zinazokwenda na mahitaji ya jamii ya sasa.
Hata hivyo, alitaja changamoto zinazowakabili, ikiwemo kutokamilika kwa ujenzi wa msikiti wa skuli, uhaba wa madarasa ya madrasa na upungufu wa vifaa vya kufundishia.
Skuli ya Asco Muslim ilianzishwa tarehe 8 Januari 2023 ikiwa na wanafunzi 10 na walimu 5. Kwa sasa skuli hiyo ina jumla ya wanafunzi 132 na walimu 10, ikitoa elimu ya maandalizi na msingi.





















