Kituo cha kulelea watoto yatima cha Assalam Orphans Centre kimefanya dua maalum ya kuiombea nchi iendelee kuwa na amani, umoja na utulivu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na The Times of Zanzibar, Mkuu wa kituo hicho, Bi Khadija Khamis Hamdani, amesema lengo kuu la dua hiyo ni kuiweka nchi mikononi mwa Allah ili iendelee kuwa na neema ya amani na mshikamano.

“Tumeamua kuomba dua hii tukishirikiana na watoto wetu yatima ili Allah atujaalie amani na utulivu katika nchi yetu, hasa kipindi hiki cha uchaguzi ambapo changamoto huwa nyingi. Tumeomba pia tupate viongozi bora wenye hofu ya Mungu,” amesema Bi Khadija.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanalelewa katika mazingira salama na yenye maadili, ambayo yanalenga umuhimu wa kudumisha amani nchini.
“Tuwe na utulivu, tupige kura zetu kwa amani. Bila amani, hakuna maendeleo. Ni jukumu letu sote kulinda utulivu huu tuliopewa,” alisema.
Nao watoto kutoka kituo hicho wamesema wamefanya dua hiyo kwa moyo mmoja, wakiiombea nchi ipate maendeleo na viongozi wenye hekima.

“Tumeomba dua kwa ajili ya viongozi wetu na nchi yetu ipate amani na furaha, maana bila amani hakuna maendeleo,” wamesema kwa pamoja.

Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa kituo hicho amesema amefurahishwa na hatua hiyo, akisema kuwa ni mfano mzuri wa malezi mema yanayojenga uzalendo na heshima kwa taifa.
Dua hiyo imehusisha watoto yatima pamoja na walezi wao, wakiongozwa na Mkuu wa kituo hicho,ambapo dua hiyo ilianza kwa kuwaombea dua Waislamu wote waliotangulia mbele ya haki, pamoja na viongozi wa taifa waliotangulia, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu alinde taifa na wananchi wake wakati wote wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.





















