Na Fatma Rajab.
Wajasiriamali wadogo wadogo wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na wakati huo huo kuhakikisha wanawalea watoto wao katika malezi bora yenye maadili mema.
Wito huo umetolewa na Siti Abass Ali, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wakati akiendelea na zoezi la kujaza fomu za mikopo isiyo na riba kwa wanawake wajasiriamali wadogo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Siti amesema lengo la mikopo hiyo ni kuhakikisha wanawake wote wanapata mikopo isiyo na riba ili kuwawezesha kuinuka kiuchumi na kujikimu katika maisha yao ya kila siku. Amesema serikali imejipanga kuhakikisha wanawake wanapata mitaji bila masharti magumu ili kupunguza changamoto zilizokuwa zikikabili kundi hilo, hususan mikopo yenye riba kubwa maarufu kama “kausha damu.”
“Tumeanzisha mpango huu baada ya kufanya utafiti na kubaini kwamba wajasiriamali wengi walikuwa hawana uhakika wa kupata fedha au walikuwa wakipata fedha lakini hawajui pa kuzielekeza. Sasa tunawahakikishia kuwa tutawaongoza katika njia sahihi ili kupata mikopo yenye masharti nafuu,” alisema.
Aidha, Bi. Siti aliwataka wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto wao kwa misingi bora ya maadili, akisisitiza kuwa jamii yenye malezi mazuri inachangia maendeleo ya taifa. Pia aliwahimiza wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi, akisema bila amani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja, Abeda Ali Mzee, alisema lengo la mikopo hiyo ni kuwakusanya kina mama wajasiriamali ili waweze kujaza fomu na kufaidika na mpango wa mikopo uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameamua kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini kote. Kila mnufaika atapatiwa mkopo wa shilingi laki tano, atakaporejesha kiasi cha shilingi elfu thelathini kila mwezi. Lengo ni kuwaondoa wanawake katika umaskini na kuwawezesha kujiendeleza kimaisha,” alisema Abeda.

Naye Fatma Ussi Juma, Katibu wa Vikundi kutoka Wilaya ya Moga, alisema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi, hivyo akawataka wanawake wenzake wajitokeze kwa wingi kujiunga na vikundi ili kupata fursa hiyo muhimu.
“Ni wakati wa wanawake kusimama imara, kushirikiana na kutumia mikopo hii vizuri ili kubadilisha maisha yao na familia zao,” alisisitiza Fatma.
Mikopo hiyo isiyo na riba ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha uchumi wa wanawake wajasiriamali wadogo na kukuza maendeleo endelevu katika jamii.





















