Na Mwandishi wetu, TOZ.17/11/2025.
Wajasiriamali wa vikundi vya kuweka na kukopa kutoka Shehia ya Jambiani Kibigija wameiomba serikali na mashirika binafsi kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa fedha ili kuongeza ufanisi katika harakati zao za kiuchumi.
Wakizungumza na TOZ, Mwenyekiti wa Kikundi cha Haturudi Nyuma, Wanu Futari Juma, amesema licha ya jitihada wanazofanya katika kujikwamua kiuchumi, bado hawajawahi kupatiwa elimu yoyote kuhusu utunzaji wa fedha jambo ambalo limekuwa likikwamisha maendeleo ya vikundi hivyo.
“Hadi sasa hatujawahi kupata mafunzo ya namna ya kuhifadhi na kusimamia fedha. Hii inasababisha tushindwe kupiga hatua kubwa katika shughuli zetu za kiuchumi,” amesema Wanu Futari.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Shehia akimwakilisha Sheha, Ahmada Issa Rai, amethibitisha kuwa vikundi vya wajasiriamali katika shehia hiyo bado havijapewa elimu ya usimamizi wa fedha. Ameiomba serikali pamoja na mashirika binafsi kushirikiana na shehia kuwapatia mafunzo hayo kwa lengo la kuimarisha uchumi wa wanavikundi.
“Hakuna elimu yoyote ambayo wajasiriamali hawa wameipata hadi sasa. Tunaiomba serikali kupitia taasisi zake pamoja na wadau wa maendeleo kuingilia kati na kuwajengea uwezo,” amesema Ahmada Issa Rai.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Meneja wa CRDB Bank, Fatma Nassor, amesema benki hiyo imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa juu ya namna bora ya kuhifadhi na kusimamia fedha ili kuongeza tija katika biashara zao.
Ameongeza kuwa CRDB itaendelea kufikisha elimu hiyo kwa vikundi mbalimbali vilivyopo Zanzibar, huku akiwahimiza wanavikundi kufika katika matawi ya benki hiyo ili kupata mafunzo yatakayowawezesha kufikia malengo yao ya kiuchumi.
“Kupitia program zetu za utoaji wa elimu, tutaendelea kufika kwa wajasiriamali na vikundi vyao. Pia tunawasihi wafike CRDB ili wapatiwe mafunzo ya moja kwa moja juu ya usimamizi wa fedha,” amesema Fatma Nassor.
Wajasiriamali wa Jambiani Kibigija wamebaki na matumaini kuwa jitihada hizi zitafungua njia mpya ya kukuza uchumi wao na kuongeza uimara wa vikundi vyao vya kuweka na kukopa.





















