Home Uchumi Biashara VIJANA WATAKIWA KUACHA KUTEGEMEA AJIRA ZA SERIKALI

VIJANA WATAKIWA KUACHA KUTEGEMEA AJIRA ZA SERIKALI

32
0

Na Fatma Rajab

Vijana wametakiwa kubadilika na kuacha kutegemea ajira kutoka serikalini, badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo katika jamii ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Furahika Islamic Vocational Training Centre, Dk. David Msuya, wakati akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo, Darajani Souk, Mkoa wa Mjini Unguja.

Dk. Msuya amesema lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane katika kuwawezesha vijana, hususan wale ambao hawakufanikiwa kufikia alama za kuendelea na elimu ya juu, pamoja na waliohitimu vizuri lakini wanahitaji ujuzi wa vitendo.

“Tunatoa elimu bure, hatutozi ada. Mwanafunzi atachangia tu vifaa vya kujifunzia. Hii ni fursa kwa vijana wote kujitokeza ili wapate ujuzi wa fani mbalimbali na kuacha kutegemea ajira za serikali,” alisema Dk. Msuya.

Ameongeza kuwa chuo hicho kinapokea watu wa rika zote, wakiwemo wenye changamoto za kiuchumi na hata watu wenye ulemavu, kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kujifunza stadi zitakazomsaidia kujitegemea.

akitaja kozi zinazotolewa chuoni hapo ni pamoja na malezi, kompyuta, usafirishaji na ukaguzi, utawala wa hoteli, ualimu na malezi ya watoto, rasilimali watu, kilimo na ufugaji wa samaki, pamoja na kozi nyingine za vitendo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa chuo hicho, Suleiman Seif Seif, amesema chuo hicho hakina ubaguzi na kinapokea watu wa aina zote

“Serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, ndiyo maana taasisi kama hizi zimeanzishwa. Tukiunganisha nguvu kati ya walioajiriwa na waliojiajiri, nchi yetu itasonga mbele,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi wa chuo hicho, Khadija Seif Salum, amesema vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo ili kujenga mustakabali wao wa kiuchumi.

“Ni vyema vijana wakaacha kutegemea serikali. Wajifunze fani mbalimbali zitakazowapatia kipato na kuwawezesha kujitegemea,” alisema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi Masoud Hemed Nassor aliwataka vijana kutumia muda wao vizuri na kuepuka maisha yasiyo na mwelekeo.

“Muda huu ni wa kujipambania. Ukipoteza leo yako, kesho yako itakuwa dhaifu. Tumia muda vizuri ili usije kujuta baadaye,” amesema.

uwepo wa chuo hicho ni jitihada za kuwahamasisha vijana wa Zanzibar kutumia elimu ya ufundi kama ngazi ya kujikwamua kiuchumi na kijamii, huku serikali na taasisi binafsi zikiendelea kushirikiana kuhakikisha vijana wanakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here