Na Said Khamis.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imedhamiria kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika mikoa yote ya Unguja na Pemba, ikiwemo Mkoa wa Kusini Unguja, kwa lengo la kuufungua mkoa huo kimaendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Mhe. Shaaban Ali Othman, amesema hayo Muungoni, Mkoa wa Kusini Unguja, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa barabara ya Muungoni–Skuli Pwani–Duta yenye urefu wa kilomita 2.65 pamoja na barabara ya Pwani–Duta–Shashamane (Ring Road) yenye urefu wa kilomita 2.25, ikiwa ni sehemu ya Shamrashamra za kuelekea Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema uwekaji wa jiwe la msingi katika barabara hizo ni uthibitisho wa utekelezaji wa sera za maendeleo zinazomgusa kila mwananchi, kwani wafanyabiashara, wakulima, wanafunzi na wananchi kwa ujumla watanufaika kwa kuendesha shughuli zao kwa urahisi na bila usumbufu.

Aidha, Mhe. Shaaban amesema ujenzi wa barabara hizo ni juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara mijini na vijijini ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo, kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar inang’ara kwa kuwa na barabara zenye viwango vya juu.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kutainua uchumi wa wananchi wa maeneo husika na kurahisisha shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo, amewataka wananchi ambao bado hawajafikiwa na ujenzi wa barabara kuwa na subira, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha barabara zote zinajengwa. Pia amewataka wananchi kuepuka kujenga kando ya barabara ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.

Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Ali Said Bakari, amesema barabara hizo ni miongoni mwa barabara za ndani zenye jumla ya urefu wa kilomita 275.95 zinazojengwa kwa kiwango cha lami Unguja na Pemba.





















