Home Siasa UJENZI NYUMBA ZA MAOFISA NA ASKARI MAGEREZA KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI.

UJENZI NYUMBA ZA MAOFISA NA ASKARI MAGEREZA KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI.

21
0

Na Said Khamis.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Umwagiliaji na Mifugo, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amesema ujenzi wa nyumba kwa ajili ya Maofisa na Maskari wa Magereza ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya watumishi hao pamoja na kuimarisha ulinzi, usalama na amani ya nchi.

Mhe. Makame ameyasema hayo huko Hanyengwa Mchana wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za Maafisa na Maskari wa Magereza, hafla iliyofanyika katika muendelezo wa Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi na makazi ya watumishi wa umma ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Mhe. Makame amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya watumishi wa umma, hususan wale wanaohusika na ulinzi na usalama, ili kuongeza ufanisi katika kulinda amani ya nchi.

Hata hivyo, amewashukuru wadau wa maendeleo kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Ndg. Mikidadi Mbarouk Mzee, amesema mradi huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.

Ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa nyumba hizo na kusisitiza kuwa itaendelea kuboresha miundombinu kwa watumishi wa umma na wananchi kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kati, Ndg. Rajab Ali Rajab, amesema ujenzi wa nyumba hizo utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Maafisa na Maskari wa Magereza katika kulinda usalama na amani ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here