Home Jamii TUKIO LA UDHALILISHAJI WA MAITI MITANDAONI LAPATA SURA MPYA, FAMILIA, WANAHARAKATI, VIONGOZI...

TUKIO LA UDHALILISHAJI WA MAITI MITANDAONI LAPATA SURA MPYA, FAMILIA, WANAHARAKATI, VIONGOZI WA DINI WATOA NENO.

57
0

Na Fatma Rajab.

Tukio la udhalilishaji wa maiti kupitia mitandao ya kijamii limeibua hisia kali miongoni mwa wananchi wa Zanzibar, huku familia ya marehemu, viongozi wa dini na wanasheria wakilaani vikali kitendo hicho wakikitaja kuwa ni cha kinyama na kinyume cha maadili ya kibinadamu na dini.

Familia ya marehemu huyo, wakizungumza nawaandishi wa habari nyumbani kwao Kisauni, Wilaya ya Magharibi ‘B’, wamesema  licha ya kukubaliana na kifo cha mtoto wao kama sehemu ya mipango ya Mungu, wamekerwa  na kusikitishwa na kitendo cha kusambazwa kwa video ya marehemu akiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti, hatua waliyoiita kuwa ni  “udhalilishaji wa hali ya juu”.

Mama mzazi wa marehemu, Fatma Mohammed, amesema wamepokea kwa uchungu mkubwa kuona video ya mtoto wao ikisambaa mitandaoni huku akionekana akiwa amefariki.

“Tumeamini kifo chake, lakini hatuwezi kuvumilia kudhalilishwa kwa namna hii. Jamii inapaswa kufikiri kabla ya kuchukua hatua za kiholela kama hizi. Watu wanazungumza mambo yasiyo na maana na yanayoumia sana kwa familia. Mtu unakubaliana na kifo, lakini si kudhalilishwa kwa kipenzi chako mitandaoni,” alisema kwa uchungu.

Salma Ali, dada wa marehemu, naye ameonyesha hasira na majonzi makubwa, akisema wanataka haki itendeke ili tukio hilo liwe fundisho kwa watu wengine wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii.

“Tunataka haki ipatikane. Mtu aliyerekodi na kusambaza video hiyo achukuliwe hatua kali. Aone ni kwa jinsi gani ametuumiza na ajifunze, kwani mitandao ya kijamii si mahali pa kudhalilishana bali pa kujifunza na kuelimishana,” alisema.

Kwa upande wa mjomba wa marehemu, Khalfan Said Salum, amesema maneno yaliyotamkwa na mtu aliyerekodi video hiyo yalionyesha dharau na chuki binafsi.

“Mtu yule alikuwa akizungumza maneno ya kashfa akimuonesha kwa kidole marehemu na kusema ‘huyu anastahili kuwekwa chini’. Neno hilo halinitoki kichwani. Hii siyo tu dharau bali ni udhalilishaji mkubwa. Tunataka kujua ni nani alifanya hivyo na kwa sababu gani,” alisema.

Mama mdogo wa marehemu naye ameongeza kuwa kitendo hicho kimewasababishia maumivu makubwa, akisisitiza kuwa maiti inapofunikwa inakuwa imestirika, hivyo si halali mtu kuifichua na kuirekodi kwa maneno ya kejeli.

“Tumekubali qadari ya Allah, lakini tunauliza tumewakosea nini hadi mtoto wetu atendwe hivi? Huu ni unyanyasaji wa kisaikolojia kwa familia nzima. Tunataka haki ya mtoto wetu,” alisema kwa uchungu.

Kwa upande wa mtaalamu wa sheria, Nadya Mwinyi Aboud, msaidizi wa sheria kutoka Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Zanzibar (ZAPAO) na mjumbe wa Mtandao wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mitandaoni chini ya TAMWA Zanzibar, amethibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa familia ya marehemu.

“Nilipokea taarifa rasmi kutoka kwa familia, nikaenda kufuatilia hatua walizochukua. Wamekwenda hospitali, kituo cha afya na kutoa taarifa polisi kituo cha Madema. Niliridhika kwamba wamefuata taratibu zote. Kwa sasa kesi ipo hatua ya upelelezi na jeshi la polisi kupitia kitengo cha makosa ya kimtandao kimefanikiwa kuizuia video hiyo kuendelea kusambaa,” alifafanua.

Nadya ameongeza kuwa tukio hilo ni ukiukaji wa sheria za makosa ya mtandao na linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wake ili kutoa fundisho kwa jamii.

“Madhara ya kutumia vibaya mitandao ni makubwa. Muathirika si marehemu pekee, bali familia, watoto wake na jamii inayomzunguka. Jamii ijifunze kutumia mitandao kwa manufaa, si kwa kuumiza wengine,” alisema.

Sheikh Shaaban Salim Humud, Mkuu wa Divisheni ya Utatuzi wa Migogoro katika Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar na mjumbe wa Baraza la Maulamaa Zanzibar, alitoa tamko kali kuhusu tukio hilo, akisema kwamba ni kosa kisheria na dhambi kubwa kimaadili na kidini kumpiga picha mtu bila ridhaa yake, hasa ikiwa ni maiti.

“Ni kosa kubwa sana kisheria na kidini kumpiga mtu picha bila idhini yake, na ni kosa kubwa zaidi kuchukua picha ya maiti hata kama ni ndugu yako wa damu. Kumkashifu maiti bila sababu ya dharura ni dhambi, na anayefanya hivyo analazimika kutubu kwa dhati kwa Mwenyezi Mungu,” alisema.

Sheikh Shaaban ameongeza kuwa toba ya dhambi kama hiyo inapaswa kufanyika hadharani kwa sababu kosa lenyewe limefanywa hadharani.

“Dhambi iliyofanywa wazi na kuharibu heshima ya mtu hadharani, toba yake pia ni lazima iwe wazi. Mtu huyo anatakiwa kuomba radhi kwa Mungu na pia kwa familia iliyodhulumiwa. Ikiwa familia haitamsamehe, basi hata Mwenyezi Mungu hatamsamehe mpaka haki irudishwe,” alisisitiza.

Kwa sasa, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku familia ikiendelea kusisitiza kuwa hawataridhika hadi haki ya marehemu ipatikane.

Ikumbukwe kuwa tukio hilo lilitokea Agost 30 mwaka huu 2025, baada ya ajali ya gari iliyosababisha vifo vya watu watatu.

Toa maoni yako ikiwa unafahamu kuwa kumpiga picha mtu bila ruhusa yake ni kosa kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here