Home Jinsia RAIS DKT. MWINYI AJUMUIKA NA WAUMINI KATIKA DUA MAALUMU YA KULIOMBEA TAIFA...

RAIS DKT. MWINYI AJUMUIKA NA WAUMINI KATIKA DUA MAALUMU YA KULIOMBEA TAIFA Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

25
0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anajumuika na Walimu wa Madrasa, Masheikh, pamoja na Uongozi wa Afisi ya Mufti Mkuu katika Dua Maalumu ya kumuombea yeye pamoja na kuliombea Taifa na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Dua hiyo inaandaliwa na Afisi ya Mufti kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kuendeleza Walimu wa Vyuo vya Qur’an Zanzibar (JUKUWAVOQUZA), na inafanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi anawakumbusha wananchi umuhimu wa kuliombea Taifa amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa amani ni nguzo ya maendeleo na ustawi wa taifa.

“Amani ni msingi wa maendeleo. Hakuna jambo muhimu zaidi kwa Taifa letu kuliko kuilinda na kuidumisha daima,” anasema Dkt. Mwinyi.

Aidha, anawahimiza viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari kutumia nafasi zao kuhubiri amani na umoja wa kitaifa wakati wote, bila kujali tofauti za kisiasa au kijamii.

Rais Dkt. Mwinyi pia anapongeza kuanzishwa kwa Jumuiya ya Walimu wa Madrasa, na anawataka wanachama wake kudumisha umoja, mshikamano na utendaji wenye kuzingatia maadili ya dini.

Akiwa katika hafla hiyo, Dkt. Mwinyi anaahidi kulivalia njuga suala la maslahi ya walimu wa madrasa katika awamu yake ijayo ya uongozi, ili kuhakikisha walimu hao wanatambuliwa rasmi na kupata mazingira bora ya kufundishia na kuendeleza taaluma ya Qur’an visiwani Zanzibar.

“Walimu wa madrasa ni nguzo muhimu katika malezi ya kiroho na maadili ya jamii. Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili kuhakikisha dhamira ya kukuza elimu ya dini inafanikiwa,” anasisitiza Dkt. Mwinyi.

Dua hiyo inashirikisha viongozi mbalimbali wa dini, walimu wa madrasa kutoka mikoa yote ya Zanzibar, pamoja na wananchi waliohudhuria kwa wingi kumuombea Rais na kuliombea Taifa kudumisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here