Home Uncategorized POLISI WAKAMATA WATUHUMIWA 17 WA WIZI WA PIKIPIKI ZANZIBAR

POLISI WAKAMATA WATUHUMIWA 17 WA WIZI WA PIKIPIKI ZANZIBAR

27
0

Na Fatma Rajab.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limefanikiwa kuwakata 17 kwa tuhuma za wizi wa pikipiki ndani ya maeneo mbali mbali ya Jiji wa Zanzibar.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna msaidizi wa Polisi Richard Thadeo Mchomvu ameyasema hayo leo Jumatano 15-10-2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Muembe Madema Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kamanda Mchomvu amesema jeshi la polisi limefanya msako maalum ulioshirikisha mikoa mitatu yote ya Zanzibar ambapo kwa maeneo mbali mbali wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao. Aidha amesema jeshi hilo limefanikiwa kwa asilimia kubwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao wamekiri kuhusika kwa wizi huo.

Kamanda Mchovu ameeleza kuwa katika watu hao kuna wengine wanahusika na wizi wa moja kwa moja na wengine wanahusika kwa kununuwa honda hizo za wizi na kuzibadilisha namba za usajili. Pamoja na Hayo amefahamisha kuwa jeshi hilo limebaini kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanafanya uhalifu huo kwa kughushi kadi ya honda ambao hazipo katika mfumo wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA na kutolewa kadi za usajili ambazo ni feki.

Kamanda MChomvu amewataka wananchi ambao wameibiwa vyombo vyao vya moto kufika katika kituo cha polisi madema kwa ajili ya kuvitambua vyombo vyao pamoja na kadi zao za umiliki.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na wanunuaji wa pikipiki za wizi akiwemo Suleiman Ramadhani Mwinyi maarufu Eddo mwenye umri wa miaka 27 mkazi wa Magogoni, Thabit Mohd Zuberi maarufu Thabi mwenye miaka 19 mkazi wa Chuini, Sharifu Juma Hamadi maarufu Mwarabu mwenye miaka 31 mkazi wa Chunga Fuoni, Juma Mohd Chuma mwenye miaka 33 mkazi wa Amani Fresh, na Abdul-Rahman Mussa mwenye miaka 25 mkazi wa Kwa Mchina Mwisho.

Kwa upande wa wezi wa pikipiki waliokamatwa ni pamoja na Abrahamani Juma Shaibu maarufu Man Mdogo mwenye miaka 20, Alkram Haji Ali maarufu Kasongo mwenye miaka 19, Abubakari Mussa Kifani maarufu Abuu mwenye miaka 22, Khamisi Juma Hassan mwenye miaka 21, Nasri Suleiman Abdalah mwenye miaka 20, Hassan Said Hassan maarufu Kaba mwenye miaka 30, Said Masoud Omary maarufu Fela mwenye miaka 31, Juma Khamisi Juma maarufu Kiboring mwenye miaka 31, Mohd Khamisi Juma mwenye miaka 24 na Abdilah Khamisi Othman maarufu Folani mwenye miaka 23. Wengine wawili waliokamatwa ambao wanajihusisha na wizi pamoja na ununuzi wa pikipiki hizo za wizi ni Khamis Abdalah Juma maarufu Bata Boy mwenye miaka 23 na Abrahman Yussuph Mmadi maarufu Kipanya mwenye miaka 20.

Jeshi la Polisi limezitaja baadhi ya pikipiki zilizopatikana kuwa ni Click mbili zenye rangi nyeupe, Vespa mbili zenye rangi nyeusi na chocolate, pamoja na pikipiki 19 za aina ya TVS zenye namba mbalimbali za usajili ikiwemo Z.513 KW, Z.931 PS, Z.443 NM, Z.899 PY, Z.546 NJ na nyengine ambazo hazina namba za usajili.

Nao baadhi ya wananchi ambao wameibiwa honda zao wamelishukuru jeshi la polisi kwa kazi kubwa walioifanya la kuwakamata wahalifu hao huku wakiliomba jeshi hilo kuongeza juhudi katika kupambana na matukio ya uhalifu hasa wizi wa vyombo vya moto.

.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here