Home Lifestyle Afya Mvua za Vuli Zafichua Changamoto za Usimamizi wa Taka Tomondo.

Mvua za Vuli Zafichua Changamoto za Usimamizi wa Taka Tomondo.

22
0

Na Hapsa Juma.17/11/2025.

Katika siku hizi za mvua za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya Zanzibar, suala la usimamizi wa taka limekuwa mjadala mkubwa katika kijiji cha Tomondo, wilaya ya Magharibi “B”. Mvua hizi huambatana na changamoto nyingi, ikiwemo kuziba kwa mitaro na kuzagaa kwa taka, hali inayoweza kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya milipuko.

Ndani ya kijiji hiki, kila mkazi ana simulizi yake kuhusu namna anavyohifadhi taka, changamoto anazopitia na mbinu anazotumia kukabiliana na mazingira yenye unyevunyevu.

Bi. Munawwar Ali, mama wa watoto watatu, anaelezea ugumu anaokutana nao kutokana na ukosefu wa doo la taka ndani ya nyumba. Kwa sasa, analazimika kutupa taka zake moja kwa moja kwenye polo. Ingawa anajitahidi kutenganisha mabaki ya chakula na pempas ili kuepusha harufu mbaya, bado haridhishwi na huduma ya ukusanyaji taka ambayo hufanyika mara moja tu kwa wiki.

Bi. Zuhura Kombo, ambaye naye hutumia polo kama sehemu kuu ya kuhifadhi taka, anaamini kuwa usafi huanzia katika kuweka taka eneo salama. Amegundua mbinu ya kupunguza uchafu kwa kuwapa kuku mabaki ya chakula, hatua inayosaidia kupunguza taka zinazokusanywa. Hata hivyo, anasisitiza kuwa mfumo wa kukusanya taka mara moja kwa wiki hauendani na mahitaji ya sasa ya kijiji.

Kwa upande wa Bi. Salama Juma , yeye ana dasbin ndani ya nyumba lakini hutupa taka kwenye polo baada ya kujaa. Anakiri kuwa kutokuwepo kwa elimu ya kutosha kuhusu utenganishaji taka kunamfanya ashindwe kujihusisha sana na mchakato huo.

Tofauti na wengine, mama wa watoto sita, Bimkubwa, anasema huduma iliyopo ya ukusanyaji taka inamridhisha. Yeye hutumia mbinu ya kutenganisha mboga mboga na majani ya mihogo au ndizi, kisha kuwapa ng’ombe wanaowafuga. Kwa namna hiyo, hupunguza kiasi kikubwa cha taka zinazokwenda kwenye polo.

Bi. Maryam Khamis ana mtazamo wake pia. Anaona huduma ya kukusanya taka inafanya kazi vizuri, akiongeza kuwa hutenganisha mabaki ya chakula kwa kuwapa wanyama na kuchoma plastiki kabla ya kutupa taka zingine kwenye polo.

Lakini hali iko tofauti upande wa uongozi. Mjumbe wa Sheha wa Tomondo, Hassan Kipanga Abdallah, anaeleza wazi kuwa bado kuna changamoto kubwa ya nidhamu ya kuhifadhi taka.

“Wengi hawatenganishi taka wanachanganya kila kitu kwenye polo. Pia wapo wanaotupa taka majiani au kuwapa mifugo wazitupe hovyo,” anasema.

Amefafanua kuwa serikali imeweka utaratibu maalum wa kukusanya taka kila Jumamosi kwenye vituo vilivyopangwa, na kisha kuzipeleka jaa kuu la Kibele. Pamoja na hilo, kuna wananchi wanaoendelea kukaidi taratibu, hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wa Manispaa ya Magharibi “B”, Bi. Aisha Felisian Benard amethibitisha kuwa uhaba wa magari ni changamoto kubwa, lakini bado wanafanya kila jitihada kushirikiana na vikundi vya usafi kuhakikisha taka zinaondolewa mara kwa mara katika maeneo yote.

Aidha, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaotumia mvua kama kisingizio cha kutupa taka hovyo.“Kutupa taka kwenye maji ya mvua husababisha mitaro kuziba na kuongeza hatari za mafuriko na magonjwa,” amesema Bi. Aisha.

Msimu wa mvua za vuli ukiendelea, Tomondo linabaki kuwa shehia yenye sura mbili, kuna wale wanaojitahidi kulinda mazingira kadri ya uwezo wao, na wale ambao bado hawajachukua jukumu la kuhifadhi taka ipasavyo. Na kama tahadhari hazitazingatiwa mapema, mvua hizi zinaweza kugeuka chanzo kikuu cha maradhi ya mlipuko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here