Michamvi, Kusini Unguja Kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa wageni katika kijiji cha Michamvi kumeelezwa kuwa moja ya sababu kubwa ya kuporomoka kwa maadili miongoni mwa vijana wa eneo hilo.
Baadhi ya wazazi na walezi wa kijiji hicho wameeleza kuwa vijana wamekuwa wakiiga tamaduni za watu wanaoingia kijijini hapo kutoka maeneo mbalimbali, jambo ambalo limesababisha kuachana na mila na desturi za Kizanzibari.
Wamesema wageni hao wamekuwa wakiishi bila kujistiri na kujihusisha na shughuli zisizofaa kijamii, hatua ambayo imekuwa ikiwapotosha vijana wa kike na wa kiume katika maadili.

“Watoto wetu sasa wameharibika kimaadili. Wamekuwa wakiiga mavazi, maneno na tabia za hawa wageni. Wengi wao hawana heshima, na hata wakielekezwa, hutoa maneno yasiyofaa. Hali hii inatukatisha tamaa sisi wazazi kwa sababu vijana wetu hawasikii tena,” amesema mmoja wa wazazi wa kijiji hicho.
Wengine wameeleza kuwa wageni wanaoingia kijijini hapo wamekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia, ikiwemo ndoa kuvunjika kutokana na tamaa na vishawishi vinavyotokana na wageni hao.
“Tumekuwa tukipokea kesi nyingi za wanawake kuachwa au wanaume kuacha wake zao kwa sababu ya wageni hawa. Hatujisikii salama tena. Tunaomba mamlaka zifuatilie jambo hili kwa ukaribu na kuweka utaratibu utakaodhibiti mienendo yao,” ameeleza mlezi mmoja wa Michamvi.
Kwa upande wake, Kazija Hassan Thabiti, Mjumbe wa Sheha wa Shehia ya Michamvi, amesema hali ya kuporomoka kwa maadili kijijini humo imesababishwa na mienendo isiyo ya heshima ya baadhi ya wageni, ikiwemo mavazi yasiyokuwa na staha.
“Tulikuwa na kikundi cha polisi jamii ambacho kilikuwa kikidhibiti tabia hizo na kuwashauri watu wanaovaa mavazi yasiyokuwa na maadili. Lakini kwa sasa kikundi hicho kimeshindwa kuendelea kutokana na upinzani na maneno mabaya kutoka kwa wageni hao,” amesema Bi. Kazija.

Ameongeza kuwa jamii ya Michamvi imekuwa ikihimiza wadau wote, wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa na taasisi za dini, kushirikiana katika kudhibiti tabia hizo ili kulinda heshima ya jamii na mustakabali wa vijana.
Kwa upande wake, Sheikh Abdalla Mnubi Abass, Katibu wa Kamati ya Maadili ya Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, amesema kuporomoka kwa maadili ni changamoto kubwa inayozidi kuenea hasa katika maeneo ya pwani.
“Kuna vijana wengi wamekuwa wakiiga tamaduni za wageni, jambo ambalo si zuri. Hii imechangia sana uharibifu wa maadili, hasa kwa vijana wa Kizanzibari. Tunawaomba wazazi wawalee watoto wao kwa misingi ya dini na utamaduni wetu ili kuepuka athari hizi,” amesema Sheikh Mnubi.
Amezitaka mamlaka husika kuhakikisha wageni wote wanaoishi Zanzibar wanaheshimu sheria, mila, na maadili ya Kizanzibari, pamoja na kufuata misingi ya dini ya Kiislamu ili kulinda utulivu na heshima ya jamii





















