Na Tatu Jaku.
Wananchi wa Shehia ya Bungi, Wilaya ya Kati Unguja, wameiomba serikali kuingilia kati kesi ya mtoto mwenye ulemavu wa viungo aliyebakwa na kupewa ujauzito, wakihofia huenda haki yake ikacheleweshwa au kupotea.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wananchi wamesema tukio hilo limewasikitisha na kuibua hisia kali katika jamii, hasa kutokana na hali ya mtoto huyo ambaye hana uwezo wa kujitetea ipasavyo.
“Hili ni jambo la kusikitisha sana. Mtoto huyu alikuwa akihitaji uangalizi maalum, sasa kuona ametendewa ukatili wa aina hii ni uchungu mkubwa. Tunaiomba serikali isimamie kwa ukaribu ili haki itendeke,” alisema mmoja wa wananchi wa eneo hilo kwa masharti ya kutotajwa jina.
Mama mzazi wa mtoto huyo amesema awali hakujua kuwa mwanawe ana ujauzito hadi alipigiwa simu kutoka skuli na kuambiwa mtoto ameanguka na anatakiwa kufikishwa hospitali.
“Nilipofika skuli, nilimkuta mtoto wangu akiwa ofisini na walimu wake. Waliniambia ni vyema nimpeleke hospitali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (ZU) kwa matibabu. Nilipofika huko, madaktari walisema mtoto ana ujauzito, nilishtuka sana, sikuamini,” alisema mama huyo kwa huzuni.
Amesema baada ya kufika nyumbani, mtoto alimweleza kwamba mtu aliyemfanyia ukatili huo ni jirani yao aitwaye Buruhani.
“Nilipomuuliza ni nani huyo Buruhani, akanijibu, ‘alikuwa akija mara kwa mara nyumbani wakati wewe hupo.’ Nilihisi uchungu mkubwa sana,” amesema.
Mama huyo amesema mara baada ya kupata maelezo hayo aliripoti tukio hilo kwa uongozi wa skuli na kwa Sheha wa Shehia ya Bungi, na kisha kupelekwa katika kituo cha polisi Tunguu kabla ya kesi hiyo kuhamishiwa kituo cha polisi Unguja Ukuu, ambako inaendelea kushughulikiwa.
Ameongeza kuwa baada ya vipimo, madaktari wa Hospitali ya Mwera-Pongwe walithibitisha kuwa mtoto wake ana ujauzito wa miezi minne.
Kwa upande wake, mtoto aliyefanyiwa ukatili huo amesema kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa alimkuta akiwa nje ya nyumba yao kisha akamvuta hadi ndani ya jumba bovu lililo karibu na nyumba yao na kumfanyia ukatili huo.

“Sikumbuki vizuri maneno aliyokuwa akiniambia,” alisema kwa sauti ya chini.

Sheha wa Bungi, Vuai Ramadhan Vuai, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tayari mtuhumiwa yuko chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.
“Ni kweli tukio limetokea. Mtuhumiwa yuko polisi kituo cha Unguja Ukuu, na taratibu za kisheria zinaendelea. Tunawaomba wazazi wawe karibu zaidi na watoto wao, na vijana waache tabia za kudhalilisha watoto,” amesema Sheha Vuai.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia, Sabah Bakar Hassan, amesema matukio ya aina hiyo yamekuwa yakijirudia licha ya elimu kuendelea kutolewa kwa jamii.
“Kwa sasa tunashughulikia tukio hili la mtoto mwenye mahitaji maalum kubakwa na kupewa ujauzito na mtu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30. Tunaiomba jamii iendelee kupata elimu kuhusu haki za watoto na madhara ya ukatili wa kijinsia,” amesema mwanaharakati huyo.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi wa shehia na vyombo vya sheria ni muhimu ili kuhakikisha waathirika wanapata haki na wahalifu wanachukuliwa hatua stahiki.
Kwa sasa, kesi hiyo inaendelea katika kituo cha polisi Unguja Ukuu, na taarifa zinaeleza kuwa mtuhumiwa tayari amekamatwa na yupo mikononi mwa vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.





















