Na Fatma Hamad, Pemba
Katika jimbo la Ole, Kusini mwa Kisiwa cha Pemba, jina la Maryam Saleh Juma limekuwa likitajwa kwa heshima, ujasiri na matumaini mapya.A
Mwanamke huyu, ambaye safari yake ya kisiasa imepitia dhoruba nyingi, leo anasimama tena kuwania ubunge kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMA) akiahidi mabadiliko kwa wananchi wa Ole.
SAFARI YAKE KUTOKA CUF HADI CHAUMA
Maryam ana umri wa miaka 52, alianza siasa akiwa kijana kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mwanzoni mwa miaka ya 95, akijitolea kuhamasisha wanawake kushiriki katika siasa za vyama vingi.
“Nilianza kama mwanaharakati wa wanawake CUF nikiwa na matumaini kwamba mwanamke naye anaweza kusimama jukwaani bila kuogopa,” anasema Maryam.
Baada ya mvutano wa muda mrefu ndani ya chama hicho, alihama na kujiunga na NCCR Mageuzi, akivutiwa na sera za mageuzi na demokrasia ya kweli.
Hata hivyo, mazingira ya kisiasa hayakumruhusu kutekeleza malengo yake ipasavyo.
“Nilitamani kuona uwiano wa haki, lakini nikagundua bado wanawake hawapewi nafasi ya kweli,” anasema.
Mwaka 2003, Maryam aliamua kujiunga na CHAUMA, chama kinachopigania ukombozi wa wananchi kiuchumi na kijamii.
Hapa ndipo alipoamua kugombea ubunge wa Jimbo la Ole, ikiwa ni mara yake ya mwanzo kugombea nafasi hiyo kupitia chama hicho cha CHAUMA, huku akiahidi “uongozi wa uwazi, usawa na maendeleo ya wote.”
Anasema hii ni mara yake ya nne kugombea nafasi hiyo ya Ubunge, ingawa hajabahatika kuingia kwenye maamuzi.
DHORUBA YA KUKAMATWA NA KUWEKWA NDANI
Safari ya Maryam haikukosa maumivu, Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2000, alikamatwa na polisi baada ya kutoa kauli iliyolalamikia matumizi mabaya ya fedha za kijiji.
“Nilikaa ndani siku tatu,” anakumbuka kwa utulivu, “Nilitoka nikiwa na nguvu zaidi, Nilijua kuwa hii ndiyo bei ya kusema ukweli.”
Mbali ya hayo baada ya maandamano yaliyofanyika mwaka 2000, alikamatwa tena kuekwa ndani, na alipotolewa akamua moja kwa moja kutoka kwenye chama hicho na kuhamia NCCR.
Maryam Saleh Juma ni taswira ya mwanamke Mzanzibari anayekataa kunyamaza mbele ya changamoto.
Safari yake kutoka CUF hadi CHAUMA imejikita katika imani ya kuwa “mabadiliko hayaletwi na hofu, bali na ujasiri,
akiwa amekumbana na mateso, kukamatwa, na changamoto za kifamilia, bado anaamini kuwa wanawake wakisimama, jamii nzima itasima.’’
MUME WAKE
Mume wake Hamad Khamis Mwalim, anasema familia haikuwahi kukata tamaa.
“Tulimfariji, Tulijua anachopigania ni haki, na leo tumeona thamani yake kijamii imeongezeka.”
Anasema anamunga mkono kila hatua, kwani hata hizo safari zake za kwenda nyumba kwa nyumba na kupiga kampeni anampeleka kwa usafiri wake mwenyewe, ilimradi tu atomize ndoto zake.
“Tulimpoteza mara kadhaa kwa misukosuko ya siasa, ingawa leo tunamwona kama mfano wa mwanamke anayejua anachokitaka.”
Mtoto wake Ummulkhairat Suleiman Bakar anasema mayake ni mwanamke wa mfano na anafaa kuchaguliwa na kua kiongozi.
“Mama ni mfano wetu, anaonyesha kuwa mwanamke anaweza kusimama na kusema ukweli, tunaamini akishinda jimbo la Ole litan’gara kwa maendeleo.

VIPAUMBELE VYAKE KWA WANANCHI WAKE
Anasema wa wanawake vijijini kupitia mikopo midogo bila riba na mafunzo ya ujasiriamali.
Kiapaombele chake chengine ni kuweka Ofisi ya Jmbo, wananchi wafike na kupeleka kero zao, apate kuzifahamu na kuzitatua.
‘’Nitaweka Ofisi ndogo ya jimbo kila mwananchi afike apelike kero zake nipate kumsaidia,’’anasema
Kipaombele chengine ni kuweka bajeti maalumu kwa kusaidia wagonjwa ambao wanahitaji kwenda kutibiwa ndani kisiwa cha Unguja na hata nje ya nchi.
Pia anasema atahakikisha anaboresha miundombinu ya Skuli ikiwemo kuweka vifaa vya maabara, kuhakikisha wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi, ili kuzalisha wataalamu bora katika sekta ya afya.
Sambamba na hayo anasema atasimamia suala la elimu ili kuhakikisha watoto wa kike na wasichana wa Ole wanamaliza skuli bila kukatishwa masomo kutokana na kupata ujauzito ama kwa kuozeshwa.
Pia anasema ataweka utaratibu wa kuchangia vipolo viwili vya mchele na unga kila familia inayopatwa na msiba ama harusi.
Anasena atahakikisha miradi ya kijamii na fedha za maendeleo zinawanufaisha wananchi wote.
“Nataka siasa iwe chombo cha kutatua matatizo, si cha kuogopwa,” anasema Maryam.
KAULI KUTOKA KIONGOZI WA CHAUMA
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMA Mohammed Massou Rashid anamtaja Maryam kama ni nguzo ya matumaini ya wanawake wa kizazi kipya
“Ana uthubutu, anajua kujenga hoja, na anaungwa mkono na jamii yote ya Ole na hata sisi viongozi wake,” anasema.

TAKWIMU
Kwa mujibu wa ripoti za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), uchaguzi wa mwaka 2025 umeweka rekodi mpya:
Asilimia 19 ya wagombea ubunge Tanzania Bara na Zanzibar ni wanawake (ongezeko kutoka asilimia 13 mwaka 2020).
Kati yao, CHAUMA imesimamisha wanawake 24 kwa nafasi mbalimbali, ikiwemo wabunge 9 na wawakilishi 15, idadi kubwa zaidi tangu chama hicho kianze kushiriki uchaguzi mwaka 2015.
Kwa Zanzibar pekee, wanawake wagombea wameongezeka kutoka 27 mwaka 2020 hadi 41 mwaka huu 2025, wengi wakitoka vyama vidogo kama CHAUMA, ADC na ACT-Wazalendo.
MIKATABA
Mikataba ya kimataifa kama CEDAW (1979) na Katiba ya Zanzibar (Ibara ya 21 na 25) inatambua haki ya kila mwanamke kushiriki kikamilifu katika uongozi wa nchi, jambo ambalo Maryam anasema ni msingi wa mapambano yake.
“Haki ya mwanamke kushiriki si zawadi, ni wajibu wa katiba,” anasisitiza Maryam.
|MTAZAMO WA JAMII
Wananchi wa Ole wanamwona Maryam kama kioo cha matumaini. mwenye utu na kujali watu wengine.
“Anasema bila woga, anaishi kama sisi, anajua shida zetu,” anasema Bi Asha Ali Khamis mkaazi wa Uwandani.





















