Wito umetolewa kwa jamii kuyatumia mabaraza ya Vijana ngazi ya Shehia kuwa ni njia ya kuwasaidia Vijana kujitambua na kuepuka kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na vitendo viovu.
Akizungumza Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan huko Shehia ya Mtowapwani Wilaya ya Kaskazini A katika Mkutano wa Baraza la Vijana Shehia ya Mtowapwani amesema ni vyema kwa jamii kutambua lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Baraza la Vijana Zanzibar.
Amesema endapo Vijana watajiunga na Baraza la Vijana watapata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujengewa uwezo wa kujitegemea, kujikwamua kiuchumi na kuwaandaa kuwa Viongozi bora wa baadae.
Akizungumzia suala la mashirikiano amesema ni vyema kwa jamii na Viongozi wa ngazi mbali mbali kuyapa mashirikiano mabaraza ya Vijana katika maeneo yao hali itakayowasaidia Vijana kupata fursa mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Aidha, ametoa wito kwa Vijana hao kuhakikisha wanailinda amani ya Tanzania ili kuisaidia Serikali kupanga mikakati ya kuwaletea maendeleo Wananchi wa Tanzania akisema Uwepo wa Amani Nchini ndio urithi wa vizazi vya sasa na baadae.
Kwa upande mwengine Katibu huyo ameyataka Mabaraza ya Vijana ya Shehia zote za Zanzibar kuiga mfano kwa baraza hilo kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa mabaraza kwa ngazi za Shehia

Akitaja mafanikio Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Shehia ya Mtowapwani Mohammed Juma Ali amesema Uwepo wa Baraza la Vijana katika Shehia hiyo umewafikia Vijana 32 walioathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya na watatu kati ya hao kuacha na kuwa Vijana wema.
Aidha Baraza hilo limefanikiwa kutoa elimu ya udhalilishaji na ukatili kwa watoto wapatao wapatao 98 sambamba na kuwafikia Vijana 106 na kuwajengea uelewa wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Zanzibar ya mwaka 2023
Mafanikio mengine ni pamoja kuanzisha miradi ya Kilimo, utunzaji wa Mazingira ya bahari na urejeshaji wa mikoko na kuanzisha Kampeni ya kuwarejesha watoto Skuli kwa wale walioacha Skuli.
Akizitaja changamoto zinazowakabili Vijana wa Shehia hiyo ni pamoja na ongezezeko la Vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya hali inayoathiri jamii ya hapo na Taifa kwa ujumla
Ukosefu wa Ofisi ya kudumu kwa baraza hilo na kukosa mashirikiano kwa baadhi ya wanajamii imekuwa ni kikwazo cha kufikia malengo waliojiwekea kwa asimilia zote.
Akitoa neno la Shukran Diwani wa Wadi ya Kipange Khamis Kombo Khamis amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Husein Ali Mwinyi kwa kuanzisha Wizara ya Vijana ili kuhakikisha Vijana wanapata fursa mbalimbali zitawasaidia kujiajiri na kutoa mchango wao wa kuiletea maendeleo Zanzibar.
Aidha amesema atahakikisha mabaraza ya Vijana yaliyomo ndani ya Wadi anayoiongoza yanapewa ushirikiano mkubwa na Viongozi wa Jimbo hilo





















