Home Jamii MAADHIMISHO SIKU YA MTOTO WA KIKE: WAZAZI WATAKIWA KUTATHMINI MALEZI NA CHANGAMOTO...

MAADHIMISHO SIKU YA MTOTO WA KIKE: WAZAZI WATAKIWA KUTATHMINI MALEZI NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKUMBA WATOTO WA KIKE

78
0

Na Fatma rajab.

Ni muhimu wazazi na watoto wa kike kukaa pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakumba ili watoto waweze kueleza matatizo wanayokutana nayo, hasa yanayohusiana na udhalilishaji na ukatili wa kijinsia. ushauri huo umetolewa na Siti Abas Ali, Mkurugenzi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,wakati akizungumza na wanafunzi wa kike katika shule ya Uzini, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani.

ameeleza kuwa mazungumzo ya wazi kati ya wazazi na watoto ni nguzo muhimu ya malezi bora na kinga dhidi ya vitendo vya ukatili. huo

Aidha, alisema serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha masuala ya ukatili dhidi ya watoto wa kike na wanawake yanapungua kwa kasi. Alibainisha kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2011 imeweka misingi ya haki na wajibu wa mtoto, ikiwemo malezi bora na ulinzi dhidi ya ukatili. Serikali, kupitia vituo vya huduma vya mkono kwa mkono (One Stop Centres), imehakikisha wahanga wa ukatili wanapatiwa huduma za haraka za vipimo, matibabu, na ushauri nasaha. Pia, waratibu katika shehia mbalimbali wamepewa jukumu la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa sheria hizo kwa karibu.

Kwa upande wake, Afisa wa Mipango kutoka Wilaya ya Kati, Ali Omar Hamad, alisema kupitia programu ya Mwanamke Jasiri, serikali inalenga kuwawezesha watoto wa kike na wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi, afya ya uzazi, na masuala ya usawa wa kijinsia. Alisema wanashukuru wadau wa maendeleo na wataalamu wa masuala ya watoto Zanzibar kwa kuunga mkono juhudi hizo ambazo zinalenga kuhakikisha mtoto wa kike anafikia malengo yake.

Naye Mussa Mbwara, kutoka Taasisi ya Pamoja Youth Initiative, alisema taasisi hiyo inalenga kumsaidia kijana kujitambua na kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii. Alisema, “Leo tumejitokeza kusherehekea Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, tukisisitiza umuhimu wa binti jasiri katika jamii. Tunaendesha programu nyingi zinazowahusisha vijana ili kuwajenga kuwa imara na wenye maadili.”

Wanafunzi kutoka Shule ya Uzini Sekondari walisema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa changamoto zinazowakabili watoto wa kike na namna ya kuzitatua. Pia, walitoa ahadi ya kuwa mabalozi wa kupinga ukatili kwa wanawake na watoto, pamoja na kuhamasisha wenzao kujiunga na baraza la watoto ili kujifunza na kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao.

Maadhimisho haya yameendelea kuibua hamasa kubwa miongoni mwa wanafunzi na wazazi kuhusu umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike, kumpa elimu bora, na kumjenga katika msingi wa ujasiri na utu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here