Home Lifestyle Afya KUKAMILIKA KITUO CHA AFYA RAHALEO, MKOMBOZI HUDUMA ZA AFYA.

KUKAMILIKA KITUO CHA AFYA RAHALEO, MKOMBOZI HUDUMA ZA AFYA.

20
0

Na Said Khamis.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amewataka madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya Rahaleo kutoa huduma za matibabu kwa muda wote ili kuimarisha afya za wananchi.

Waziri Suleiman ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Rahaleo, Wilaya ya Mjini, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho utakuwa mkombozi mkubwa katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Zanzibar, akieleza kuwa wananchi wengi hufuata huduma katika kituo hicho kutokana na umahiri na ubora wa huduma zinazotolewa.

Aidha, Mhe. Suleiman amewahimiza wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili iendelee kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wote.

Vilevile, ameuagiza uongozi wa Wizara ya Afya kufanya tathmini ya kina ya mpango wa uendeshaji wa kituo hicho pamoja na kuweka mpango mzuri wa matumizi ya rasilimali, ili kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi na kuboresha utoaji wa huduma. Pia amewataka wakandarasi kuongeza juhudi ili ujenzi wa kituo hicho ukamilike kwa wakati.

“Nawaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kukitunza kituo hiki, hususan katika suala la usafi, na kuhakikisha kinakuwa katika hali nzuri muda wote pindi kitakapokamilika,” amesisitiza Waziri Suleiman.

Akitoa taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Amour Suleiman, amesema Serikali imeamua kujenga vituo vya afya katika Wilaya zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kuimarisha huduma za afya, kupunguza vifo pamoja na maradhi ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Ameeleza kuwa Kituo cha Afya Rahaleo kitatoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Rahaleo na maeneo ya jirani, ikiwemo huduma za wagonjwa wa dharura na wagonjwa wa rufaa kutoka vituo vya afya vya daraja la kwanza, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.

Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni nne (4), fedha zilizojumuisha ujenzi wa jengo moja la ghorofa tano (5) lenye maeneo saba (7) ya huduma mbalimbali za afya

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here