Na mwandishi wetu.
Jamii imetakiwa kuendelea kuzingatia na kuheshimu maadili pamoja na kanuni za dini ya Kiislam wanapohudhuria misibani, ili kuondoa changamoto zinazoendelea kujitokeza katika matukio hayo.
Ushauri huo umetolewa na Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Sheikh Thabit Normal Jongo, wakati alipokuwa akizungumza na TOZ, kutokana na tabia za baadhi ya watu kutumia eneo la msibani kutangaza biasha ra na kuuza, jambo ambalo amelitaja kuwa ni kinyume na maadili ya dini ya kiislamu.
Aidha amesisitiza kwamba kila Muislam ana wajibu wa kuutukuza msiba kwa kufuata mafunzo ya dini badala ya kufanya shughuli zisizoendana na mazingira ya msiba.
Amesema kuwa misiba ni sehemu ya ibada, na kutafakari, hivyo kitendo cha baadhi ya watu kutumia maeneo hayo kwa mazungumzo yasiyo na maana au kusambaza shughuli za biashara hakikubaliki na pia ni kinyume na misingi ya dini ya Kiislam.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa hali ya misiba kubadilika na kuwa uwanja wa mazungumzo yasiyo na manufaa inaleta taswira mbaya, huku wengine wakilalamikia vitendo vya baadhi ya watu kuuza bidhaa misibani na kupunguza utulivu unaotakiwa wakati wa Ibada hiyo muhimu.
Wananchi hao wameiomba jamii kurejea maadili ya Kiislam na viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya dini na maadili, ili kurejesha heshima katika matukio ya misiba ambayo hugusa hisia na maisha ya watu wengi.





















