Home Jamii ELIMU YA UDALILISHAJI WA KIJINSIA YASAIDIA KUPUNGUZA VITENDO VYA UNYANYASAJI KWA WANAWAKE...

ELIMU YA UDALILISHAJI WA KIJINSIA YASAIDIA KUPUNGUZA VITENDO VYA UNYANYASAJI KWA WANAWAKE NA WATOTO MICHAMVI.

68
0

Na Fatma Rajab , Kusini Unguja.

Utolewaji wa elimu kuhusu udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto umeelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya unyanyasaji katika kijiji cha Michamvi, mkoa wa Kusini Unguja.

Wakazi wa kijiji hicho wamesema kuwa elimu hiyo imewasaidia kuelewa namna ya kukabiliana na vitendo hivyo, sambamba na kuwafundisha watoto njia bora za kujilinda na kuripoti matukio wanayokutana nayo.

“Mafunzo tunayopokea yamekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Sasa tunakaa na watoto wetu mara kwa mara, tunawafahamisha kuhusu dalili za udhalilishaji na kuwaelekeza kuwa wakiona viashiria vyovyote, waripoti mara moja kwa wazazi au walezi wao,” alisema mmoja wa wanakijiji.

Wameeleza pia kuwa elimu hiyo imewasaidia wazazi kuboresha malezi ya watoto kwa kuzingatia mazingira rafiki na ya kuaminiana, jambo linalorahisisha watoto kueleza changamoto wanazokutana nazo bila woga.

“Watoto wanaolelewa katika mazingira yasiyo rafiki huwa na hofu ya kusema ukweli pale wanapodhalilishwa. Lakini sasa, kutokana na elimu hii, tumejifunza kuwajenga kisaikolojia ili wajue kuwa wazazi ni sehemu salama ya kueleza matatizo yao,” aliongeza mzazi mmoja.

Kwa upande wake, Kazija Jaku Vuai, Mratibu wa Wanawake na Watoto wa Shehia ya Michamvi, amesema juhudi za utoaji elimu zimekuwa zikiendelea kwa kupitia mikutano ya shehia na ziara za nyumba kwa nyumba, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wazazi na walezi kuhusu namna ya kulinda watoto dhidi ya udhalilishaji.

“Tumeona mabadiliko makubwa. Wazazi na walezi wamekuwa na mwitikio mzuri sana wanahudhuria mikutano, wanapokea elimu kwa moyo na wanaifanyia kazi. Kwa sasa, matukio ya udhalilishaji yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kijiji chetu,” alisema Bi. Vuai.

Aidha, amewataka wazazi kuendelea kuwa karibu na watoto wao, kuwapa elimu ya kujitambua na kuripoti mara moja endapo kutatokea dalili zozote za udhalilishaji.

“Vitendo vya udhalilishaji havina nafasi katika jamii yetu. Ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto analelewa katika mazingira salama na yenye upendo ili kuepusha madhara ya kimwili na kisaikolojia,” amesisitiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here