Na mwandishi wetu .
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amewahimiza Wananchi, na hasa waumini wa dini ya Waislamu kuzingatia Misingi ya Malezi ya Kiimani, katika kulinda amani na ustawi wa Jamii, ili kulinusuru Taifa.
Alhaj Othman ameyasema hayo leo Novemba 07, 2025, alipojumuika na Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi, katika Sala ya Ijumaa, hapo Masjid Mwitani, Msikiti uliopo Mtemani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mheshimiwa Othman amesema kuwa kilichotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni, Vijana wadogo, walitumiwa kuhujumu haki, nje ya Miongozo na Misingi ya Dini ya Kiislamu.
“Mnapokubaliana na mkaweka Miongozo yenu kama Binaadamu Wastaarabu, hata kama haipo ndani ya Msahafu, pindipo wakitokea Watu wakaikiuka, hiyo inakuwa ni dhulma, na Mwenyezi Mungu katu Haikubali”, amesema Mheshimiwa Othman akieleza yale yaliyotendeka yakiwemo ya kupora Uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni Nchini kote.

Amefahamisha kwamba takriban Chaguzi zote zilizotangulia hapo kabla, palishuhudiwa Watu walioongoza hujuma na mauaji, kwa kiasi kikubwa walitokea nje ya Zanzibar, bali uporaji wa mara hii uliwahusisha, wenyewe- kwa-wenyewe kutoka Unguja na Pemba.
“Moja, kubwa ambalo tumelipata mara hii, Mwenyezi Mungu Ametubainishia kuwa hujuma na uovu wameutenda wenyewe Ndugu zetu, Watoto wetu, Kaka zetu, Ami zetu, Shangazi zetu au Dada zetu, kutoka hapa hapa kwetu”, amesema.
Amesema, laiti kama Jamii hii ambayo Viongozi wake kwa asilimia kubwa ni Waislamu, wangelisimamia kwa kufuata Miongozo ya Haki, Imani na Malezi yenye Maadili, ingelikuwa ajabu kuona dhulma na hujuma za kiutawala, wanazokutana-nazo wananchi wasiokuwa na hatia, zikitendeka mfululizo kiasi cha kuushangaza Ulimwengu hata kwa Wasiokuwa-Waislamu.
“Ifike hatua katika Nchi yetu hii, zikifika nyakati za uchaguzi kusiwe na hofu, mashaka, wasiwasi wala taharuki”, ameeleza Alhaj Othman akihimiza umuhimu wa amani ya kweli hapa Nchini.
Amebainisha kwamba, tatizo kubwa ni kutofuata Miongozo ya Dini, Imani, Malezi, pamoja na Mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW); na badala yake baadhi ya Watawala kuzingatia mno maslahi binafsi ya kidunia, huku akisema kinachoonekana sasa ni “ukimya wa khofu, na siyo amani”.

Aidha, Mheshimiwa Alhaj Othman amebainisha kwamba kilichotokea katika Uchaguzi huo, yanapaswa kuleta mazingatio ya kiimani, na wala siyo ya kufumbiwa macho, kwa kile kinachoonekana ni amani ya woga.
Aidha amefahamisha kwamba, kinachotakiwa ni kutafutwa suluhisho la kudumu ili kuwa na utulivu, haki na amani ya kweli, inayojali malezi na maadili bora, hasa kwa vijana na vizazi vijavyo.
Hivyo, Mheshimiwa Othman ametahadharisha mwenendo huo, ambao amesema unazalisha ‘uheshimiwa na waheshimiwa wa kinafiki’, huku Wananchi katika nyoyo zao wakiamini kwamba Vyeo hivyo ‘ni feki’, vimepatikana kwa njia na misingi ya batili, dhulma na haramu.
Pamoja na yote hayo, Mheshimiwa Othman amerudia ahadi yake kwamba, yeye na Viongozi wenzake, ambao Umma Mkubwa wa Wananchi wengi uliwachagua kwa kuwapigia kura nyingi za Ushindi, kupitia Uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni, watahakikisha wanapigania na kutetea haki hiyo iliyoporwa, kwa njia zote za hikma, na ili khatimaye kujenga Misingi ya Amani ya Kweli na ya Kudumu, kwa maslahi ya Taifa zima.
Akitoa Khutba Mbili, Khatib na Imamu wa Sala hiyo, Sheikh Ali Abdi Abeid, amesisitiza haja ya Waumini wa Kiislamu kuwa na Subra na kutokukata tamaa, hasa katika mitihani na utafutaji wa haki, kwani kufanya hivyo ni miongoni mwa Madhambi Makubwa, na pia kukengeuka Misingi ya Dini ya Kiislamu.

Khatib huyo amesisitiza akisema, “Qur-an Tukufu imetuhimiza tusikae kimya katika kupinga dhulma; tusichoke katika kutetea haki zetu; tusikate tamaa na Rehma za Allah; wala tusichupe Mipaka Yake tunapopata neema au tunapoamua kulipiza kisasi”.
Viongozi mbali mbali wa Jamii, Dini na Siasa wamejumuika na Mheshimiwa Othman katika Ibada hiyo, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Ndugu Ismail Jussa; wakiwemo pia Mratib wa Chama hicho Kisiwani Pemba, Ndugu Rashid Ali Abdalla; pamoja na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama wa Wete, Ndugu Juma Khamis Ali.
Mara baada ya Ibada hiyo Alhaj Othman amewatembelea, kuwajulia hali na kubadilishana mawazo na Masheikh Mashuhuri wa Mji wa Wete, wakiwemo Sheikh Rashid Hamad Othman wa Utaani, Sharif Ghazal Abdalla wa Selemu, na Dokta Issa Said Mohamed wa Mtemani.





















