Na Siti Ali,
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Mhe.Shaaban Ali Othman amesema Wizara ya Vijana itaendelea kusimamia katika kupata haki na maslahi ya Vijana ili kuweza kujikwamua na umasikini wa kipato.
Ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa uhamasishaji Vijana katika kujiunga na Mabaraza ya vijana ili kupata fursa ya kuchagua na kuchaguliwa katika Uchaguzi wa Shehia Wilaya hadi Taifa huko Uwanja wa Taifa Jan’gombe,Wilaya ya Mjini.
Amesema Wizara hiyo itasimamia upatikanaji wa fursa za Ajira za Serikali na sekta binafsi pamoja na kuwawezesha Vijana hao kupata mikopo ili kuendeleza Biashara zao .
Waziri Shaabani ameahidi kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa mikopo ili Kila mwenye nia ya kufanya biashara au kukuza ujuzi wake mikopo apate fursa hiyo .
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutokubali kutozwa pesa Kwa ajili ya Ajira kutokana kwamba hakuna Ajira ya Serikali wala sekta binafsi inayouzwa. kufanya hivyo ni kinyume na Sheria ya nchi .
Akitoa salamu kwa Vijana hao Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe Hassan Hafidh amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mabaraza ya Vijana wanahitaji Kiongozi atakaekuwa na maono na uthubutu wa kuwasemea Vijana wa Zanzibar.
Aidha ametoa wito kwa Vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi kwa ngazi zote na vijana kuwachagua watu sahihi ambao watakuwa msaada kwao katika kutatua changamoto za Vijana.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana Ajira na Uwezeshaji Salama Mbarouk Khatib amesema Mabaraza ya Vijana hayajali itikadi za vyama vya siasa jinsia wala kabila hivyo kuwataka Vijana hao kuchukua fomu za kugombania uwongozi wa mabaraza hayo.
Amesema maamuzi yote ya Serikali yatakuja kwenye Sheria na mgawanyo utakuwa sawa kati ya eneo na eneo ili kuhakikisha kwamba Vijana wote popote walipo wawe na shughuli za kufanya .

Amewataka Vijana hao kutochagua kazi iwapo ni Kazi ya stara na zenye heshima na Kwa wale waliotoroka Skuli watasimamiwa na Wizara ili kupambana na soko la Ajira .
Kwa Upande wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan amesema Mabaraza ya Vijana yameanzishwa kwa ngazi za Shehia Wilaya na Taifa ambayo yanawakilisha kundi kubwa la Vijana katika Jamii.
Amefahamisha kwamba kuwahamasisha Vijana kuwa ni sehemu ya mabaraza ya Vijana ni kuufungua ukurasa mpya kuimarisha mabaraza ya Vijana Kwa Unguja na Pemba .





















