Home Jamii
51
0

Wafanyakazi Kai Hotel Nungwi Wadai Kudhalilishwa; Waomba Serikali Ichukue Hatua.

Na Mwandishi wetu.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kai Hotel iliyopo Nungwi wameeleza kuchoshwa na vitendo vya udhalilishaji na mazingira duni ya kazi wanayodai wamekuwa wakifanyiwa na baadhi ya wakuu wa hoteli hiyo. Wakizungumza na vyombo vya habari ikiwemo TOZ kwa masharti ya kutotajwa majina yao , wameeleza kuwa hali waliyoipitia imekuwa ikiwanyima utu, usalama na heshima yao kama wafanyakazi.

Wafanyakazi hao walibainisha kuwa walilazimishwa kuishi katika mazingira yasiyo ya kibinadamu, ikiwemo kulala zaidi ya watu kumi katika chumba kimoja bila haki ya kufungua madirisha Pamoja na kunyimwa chakula cha uhakika, wakilazimika kunywa maji na kuosha vyombo chooni. Aidha, waliongeza kuwa walifukuzwa kazi mara moja endapo wangeshikwa wakila au kuosha vyombo jikoni.

Pia walieleza kwamba hawakuwa na uhuru wa kutoka nje ya eneo la hoteli bila vibali maalum, huku wakitakiwa kuandika muda wa kutoka na kuingia. Walidai hawakupatiwa mikataba ya kazi wala mishahara waliyoahidiwa. Zaidi ya hapo, baadhi ya wafanyakazi wa kike walieleza kuwa walipitia udhalilishaji wa kimwili kutoka kwa baadhi ya viongozi wa hoteli wakati wa kuomba kazi au wakiwa kazini.

Baadhi yao walieleza kukumbwa na vitendo vya ukaguzi usio wa kiutu, ikiwemo kusachiwa mabegi na hata kupekuliwa hadi kwenye nguo za ndani na wanaume, jambo waliloliona kuwa ni la kudhalilisha na lisilokubalika katika mazingira yoyote ya kazi. Vitendo hivyo, kwa mujibu wao, vilichangia kuongezeka kwa hofu na msongo wa mawazo kazini.

Kutokana na hali hiyo, jumla ya wafanyakazi kumi walichukua uamuzi wa kuondoka kazini kwa pamoja baada ya kuona hakuna uwezekano wa kupata haki zao ndani ya hoteli hiyo. Walisema kuwa wanaamini hatua yao itaibua mjadala mpana kuhusu namna wafanyakazi wanaotoka maeneo mbalimbali wanavyotendewa katika baadhi ya mahoteli.

Katibu wa Sheha wa Kiungani, Nungwi, alithibitisha kupokea taarifa hizo na kueleza kuwa udhalilishaji katika baadhi ya mahoteli ni jambo linalojitokeza mara kwa mara. Alihimiza watendaji kutokupuuza malalamiko kama hayo na badala yake kuyafanyia kazi kwa haraka ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki na usalama wanaostahili. Aliongeza kuwa tayari ofisi yake imechukua hatua za awali na itafikisha suala hilo katika ngazi husika.

Kwa upande wa uongozi wa Kai Hotel, meneja wa hoteli hiyo alikanusha madai hayo, akieleza kuwa hakuna tukio lolote la udhalilishaji lililoripotiwa rasmi kabla ya wafanyakazi hao kuondoka. Alisema hoteli bado ni mpya na taratibu za mikataba ya kazi zinaendelea kukamilishwa, huku akisisitiza kuwa wafanyakazi waliolalamika walishapewa haki zao kabla ya kuondoka. Pia alikanusha madai dhidi ya mmoja wa viongozi wa hoteli anayetajwa, akisema hajawahi kuhusishwa na tabia hizo na kwamba uongozi unaelewa vizuri madhara ya udhalilishaji wa kijinsia na uko tayari kuchukua hatua iwapo kutapatikana ushahidi.

Akizungumzia madai ya wafanyakazi hao Ofisa Kazi kutoka Kamisheni ya Kazi iliyo chini ya Wizara ya Kazi na Uwezeshaji, Mariyam Juma Simai, amesema kuwa hadi sasa hawajapokea taarifa zozote za malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa Bangaloo hiyo.

Alisema Kamisheni ipo tayari kupokea na kushughulikia migogoro yoyote ya ajira endapo itaifikia kwa utaratibu unaotakiwa kisheria.

Alifahamisha kuwa ni muhimu kwa wafanyakazi kufahamu haki zao na kufuata taratibu stahiki za utoaji wa taarifa pale wanapokutana na matatizo kazini, ikiwemo madai ya mishahara, maslahi au ukiukwaji wa mikataba na mambo mengine.

Mariyam aliwataka wafanyakazi wote wenye malalamiko kufika katika ofisi za Kamisheni ya Kazi za mikoa au makao makuu ili kuwasilisha taarifa zao kwa maandishi au kwa maelezo ya moja kwa moja kwa maofisa kazi.

Aidha, alibainisha kuwa mara baada ya malalamiko kupokelewa, Kamisheni hufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria za ajira, ili kuhakikisha haki za pande zote zinazingatiwa na kutolewa kwa uadilifu.

Alisisitiza kuwa kutokutoa taarifa kunawanyima wafanyakazi haki zao na pia kunazuia mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwajiri iwapo kutabainika ukiukwaji wa sheria za kazi.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wafanyakazi nchini kuendelea kuwa jasiri kuripoti changamoto wanazokumbana nazo, akisema Kamisheni ipo kwa ajili ya kuwalinda na kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama, yenye usawa na ya haki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here