Home Jamii ALHAJ OTHMAN MASOUD AWATOA WASIWASI WANANCHI, AHIMIZA SUBRA NA MSHIKAMANO.

ALHAJ OTHMAN MASOUD AWATOA WASIWASI WANANCHI, AHIMIZA SUBRA NA MSHIKAMANO.

24
0

Na Siti Ali. Novemba 14, 2025.

Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Mhe Alhaj Othman Masoud Othman, amewaasa Wananchi wasiwe na huzuni juu ya yale yaliyotokea hivi karibuni Nchini, na wazingatie Ukubwa wa Rehma za Mwenyezi Mungu, wakiamini kwamba haki haipotei, na dhulma katu haikubaliki.

Alhaj Othman ameyasema hayo leo Novemba 14, 2025, alipojumuika na Waumini wenzake wa Kiislamu pamoja na Wananchi, katika Sala ya Ijumaa, hapo Msikiti wa Chamboni Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema, “ni dhahiri baada ya yaliyotokea wapo wengi ambao wamehuzunika na wengine kughadhibika, bali la muhimu zaidi ni kutanguliza subra na shukran kwa imani kwamba Rehma Zake Mwenyezi Mungu ni Kubwa”.

Ameeleza kuwa lililoleta huzuni na masikitiko makubwa ni kuona wapo ambao wamepora mamlaka kwa njia za kughushi, hadaa na hila, licha ya kujileta mbele ya jamii wakijivika sura za imani na kujidai kuhimiza amani.

“Kwasababu waliofanya haya tunawajua hatuna- budi kuwafika na kuwaeleza ubaya wa waliyoyatenda, pamoja na kuwakataa kutokana na dhulma hiyo”, amesema Mheshimiwa Othman huku akihimiza subra baina ya Wananchi, sambamba na kujenga imani kwa hikma na juhudi ambazo Viongozi wanazitekeleza katika kupambania haki zao.

Aidha ameongeza kwa kusema, “tunachoomba kwenu ni mshikamano na subra; wakati huu tukiendelea kuitafuta haki yetu kwa njia za amani na utulivu, na Inshaallah itapatikana”.

Akitoa Khutba Mbili, Khatib na Imamu wa Sala hiyo, Sheikh Shaame Mbwana Shaame, amekumbusha wajibu wa waumini kutenda wema, ili kuiepusha jamii kutokana na kila aina za uovu, unaoweza kuipoteza heshima, sasa na kwa vizazi vijavyo.

“Rehma ya Mwenyezi Mungu ipo karibu na wale watendao mema, Ndugu zangu pia utu wa mwanadamu ni kutenda wema na kuepuka kila baya; hata iwapo ni yale yanayomgusa mtu, dhidi ya mtu mwengine, katika kujinufaisha na anasa za dunia”, amefahamisha Khatib huyo.

Mara baada ya Ibada hiyo Waumini wa Mskiti huo, wakiongozwa na Imamu Sheikh Ali Makame Kombo, walimuombea Dua Maalum Alhaj Othman, wakimuomba Mwenyezi Mungu Amfanyie wepesi, katika majukumu yake.

Viongozi mbali mbali wa Jamii, Dini na Siasa wamejumuika na Mheshimiwa Othman katika Ibada hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama Micheweni Maalim Rashid Khalid.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here