Home Lifestyle Afya Huduma za Kisukari Kuimarishwa Zanzibar

Huduma za Kisukari Kuimarishwa Zanzibar

21
0

Na Kaid Khamis, novema 14, 2025.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha ustawi wa wa wanaoishi na changamoto za kisukari unaimarika.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk. Salim Slim aliyasema hayo wakati akifungua kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya kisukari (DAZ) Katika maadhimisho ya siku ya kisukari duniani yaliofanyika Skuli ya Tumekuja Wilaya ya mjini unguja.

Alisema Serikali inatambua changamoto za wagonjwa wa kisukari na kuwa kupitia wizara ya afya itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zao na kuwataka kutosita kuzizungumzia changamoto nyengine wakati wowote zinapojitokeza.

“Serikali imetenga kiasi cha fedha kuwekeza katika maradhi yasiyoambukiza ili kila chnagamoto ya maradhi hayo zipatiwe ufumbuzi wa haraka” alisema

Aidha aliwasisitiza wagonjwa wa kisukari kuendelea kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs) kwani wameshapatiwa mafunzo ya kutosha kutoa huduma za awali kwa jamii inayowazunguka, na kuwasisitiza wahudumu hao kuwa na mpokezi na lugha nzuri kwani ni sehemu ya tiba kwa maradhi yeyote.

Sambamba na hayo aliwasisitiza watendaji wa kitengo cha maradhi yasioambukiza kwa kushirikiana na DAZ kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuweza kujikinga, kujilinda na kuthamini wagonjwa wa ugonjwa huo.

Akisoma risala katika kongamano hilo Naibu Katibu wa Jumuiya ya Kisukari Zanzibar (DAZ) Rukia Mgongo alisema takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 500 duniani wanaishi na ugonjwa huo na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwaka 2030 nchini Tanzania.

“Idadi ya watu wanaoishi na kisukari inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na mtindo wa maisha na ulaji wa vyakula visivyo na uwiano, ukosefu wa mazoezi pamoja na ongezeko la wenye uzito kupita kiasi.” Alisema kupitia risala hiyo

Alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar ripoti ya Wizara ya Afya (2023) inaonesha kuwa wagonjwa waliyolazwa ni 56,983 kati ya hao 1,818 sawa na asilimia 32 ni wagonjwa wa kisukari, kati ya hao 29 sawa na asilimia 3.1 walifariki dunia

Naye Mwenyekiti wa DAZ Haji Abdalla Ameir ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu ili kupunguza ongezeko la wagonjwa wapya wa ugonjwa huo.

Alifahamisha kuwa matumizi ya dawa za asili holela yanapelekea mgonjwa wa kisukari kuwa hatarini kupata maradhi mengine kama figo, na ini na kuwasisitiza kuwa makini na matumizi ya dawa hizo.

Akizungumzia kuhusu athari za kisaikolojia Mwenyekiti huyo alisema kuwa wagonjwa wengi wanakabiliwa na tatizo hilo kutokana na wasiwasi wa kupata athari zaidi za ugonjwa huo.

Wagonjwa wa kisukari walieleza kuwa kusubiri kwa muda mrefu katika vituo vya afya kupata huduma hiyo ni changamoto inayopaswa kuzingatiwa kutokana na hali zao.

Hivyo wameomba kupatiwa huduma mapema mara wanapofika vituoni ili kuepuka kukaa muda mrefu bila ya kula, na kusisitiza kuandikiwa dawa katika madaftari yao ili kutunza kumbukumbu.

Kwa upande wa watoto wanaoishi na changamoto za kisukari akiwemo Anuar Faki Ali alisema wanakabiliwa na unyanyapaa maskulini kutokana na mahitaji ya kwenda haja ndogo mara kwamara.

Alieleza kuwa hali duni ya maisha ya baadhi ya wazazi inapelekea kushindwa kuwahudumia watoto wenye changamoto hizo hasa katika masuala ya mlo stahiki.

Akiwasilisha mada ya lishe katika kongamano hilo mtaalamu wa lishe kutoka hospital ya Saifee Tanzania Esther Nyamburi aliwasisistiza kuzingatia mlo kamili sambamba na kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Maadhimisho ya siku ya kisukari duniani huadhimishwa kila ifikapo Novemba 14 ambapo kaulimbiu ya mwaka huu “Kisukari na Ustawi”. Katika kongamano hilo mada mbili zilijadadiliwa ikiwemo lishe na matibabu kwa watu wa kisukari aina ya kwanza na ya pili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here