Home Jamii JE NI IPI SABABU YA KUONGEZEKA VITENDO VYA UDHALILISHAJI ZANZIBAR? WADAU WATOA...

JE NI IPI SABABU YA KUONGEZEKA VITENDO VYA UDHALILISHAJI ZANZIBAR? WADAU WATOA TAHADHARI

23
0

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Katiba na Sheria, Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mzee Ali Haji, ameshauri kufanyika kwa uchambuzi wa kina kuhusu sababu zinazopelekea kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, ili hatua madhubuti za kupunguza matukio hayo ziweze kuchukuliwa.

Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi kutoka mikoa ya Unguja, leo Novemba 10, 2025, katika Chuo cha Polisi Zanzibar, amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi kubwa katika kuzuia, kubaini na kukabiliana na makosa ya udhalilishaji, lakini bado matukio hayo yanaongezeka.

Ameeleza kuwa kuna umuhimu wa kuchunguza kwa kina sababu za ongezeko hilo, hasa ikizingatiwa kuwa wahusika wengi wanaofanya udhalilishaji ni vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 25, huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto na vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 17. Aidha ameitaka jamii kulitazama suala hilo kwa mtazamo mpana utakaowezesha kupatikana kwa njia sahihi za utatuzi.

Kwa upande wake, Afisa Hifadhi ya Mtoto kutoka Shirika la UNICEF, Ahmed Rashid Ali, amesifu utendaji wa Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi na kueleza kuwa kuanzishwa kwa Dawati katika kila kituo cha Polisi ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika kushughulikia kesi za udhalilishaji. Amesema utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa Jeshi la Polisi ni hatua muhimu katika kuhakikisha usimamizi na ufuatiliaji wa kesi hizo unafanyika kwa ufanisi.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Zanzibar, Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Ali Mohamed Othman, amesema kumekuwa na mwitikio mdogo wa wananchi kuhudhuria vikao vya utoaji elimu kuhusu kupinga udhalilishaji, pindi watendaji wa Madawati wanapowafikia katika maeneo yao. Ametaja kuwa kundi linaloonekana kukosekana zaidi ni wanaume, ambao pia ni wahusika wakubwa katika utekelezaji wa vitendo hivyo.

Mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha jamii inashirikiana kikamilifu na vyombo vya kutekeleza sheria, ili kuzuia vitendo vya udhalilishaji, na pale vinapotokea, kuhakikisha vinapatikana ushahidi unaotakiwa kwa ajili ya hatua za kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here