Home Jamii KUSAINIWA MKATABA WA WATU WENYE ULEMAVU AFRIKA, MSINGI WA MAENDELEO JUMUISHI.

KUSAINIWA MKATABA WA WATU WENYE ULEMAVU AFRIKA, MSINGI WA MAENDELEO JUMUISHI.

22
0

Na Siti Ali.

Watu wenye ulemavu kisiwani Unguja wamesema kusainiwa na kupitishwa kwa Mkataba wa Watu Wenye Ulemavu Afrika kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutu nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Wakizungumza na TOZ mara baada ya kupata mafunzo kuhusu umuhimu wa mkataba huo katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, baadhi ya washiriki hao akiwemo Nassir Salim Ali, Jamila Borafya Hamza na Nassor Khatib kutoka Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar wamesema mkataba huo utawasaidia kujua, kutambua na kutetea haki zao kwa ufanisi zaidi, jambo litakaloongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.

”Mkataba huu ukisainiwa utakuwa kama dirisha jipya la matumaini. Utatupa nguvu ya kutambua thamani yetu, kutetea haki zetu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi,” amefafanua Borafya.

Aidha Wametoa wito kwa serikali kuharakisha mchakato wa kusaini na kuidhinisha mkataba huo ili kuwezesha mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, si tu Zanzibar bali duniani kote.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu, Salma Saadati, ambaye pia alikuwa mwasilishaji mkuu katika mafunzo hayo, ameipongeza Jumuiya ya Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Kusini kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu na kusema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu itifaki hiyo na kuhamasisha jamii kuelewa nafasi yake katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu.

“Mkataba huu ukisainiwa utakuwa chachu ya mabadiliko makubwa. Tunataka watu wenye ulemavu watambulike, wapewe fursa sawa na wajisikie salama katika kila hatua ya maisha yao” amefafanua Salma.

Sambamba na hilo Salma alibainisha kuwa Baraza litaendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuiomba serikali kuhakikisha mkataba huo unasainiwa, akisisitiza kuwa utekelezaji wake utaleta mabadiliko chanya katika ustawi, hadhi na fursa za watu wenye ulemavu Afrika.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Watu Wenye Ulemavu kupitia Kikundi cha Wanawake Kusini Unguja, kwa lengo la kuongeza mwamko na uelewa kuhusu umuhimu wa mkataba huo kwa jamii na taifa kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here