Na Fatma Hamad, Pemba.
Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Hamad Rashid Moh’d ameishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)pamoja na vyama vya siasa, kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ili wapate haki yao ya kupiga kura bila vikwazo.
Mgombea huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na TOZ kwa njia ya simu, amesema maranyingi kundi la Watu Wenye Ulemavu limekua likipata changamoto juu masuala mazima ya uchaguzi.
Amesema ni vyema kwa uchaguzi wa mwaha huu 2025, kuwangaliwa kwa ukaribu kwa kuwekewa vifaa ama wakalimani, katika vituo vya kupigia kura kuona, nawao wanafika na kuchagua viongozi wao wanao wataka.

‘’Naomba tuwaangalie hawa wenzetu nawao ni binadamu kama sisi, wanahaki ya kuchagua viongozi wawatakao, tuwawekeni mazingira ambayo hayatowakosesha haki yao hiyo,’’amesema.
Nasra Fakih Hassan mwanamke mwenye ulemavu wa viungo mzaliwa wa Kangagani Wete Pemba, ambaye mwaka huu amejitosa kugombea nafasi ya uwakilishi viti maalumu, amesema mchakato wa uchaguzi umewaonesha matumaini, ingawa bado unahitaji mageuzi kwao.
‘’Mara hii kidogo tunashukuru na ndio maana wanawake wengi wenye ulemavu tumejitokeza kuchukua fomu na kuwania nafasi mbali mbali za uongozi si hayo tu bali ukiangalia hata kwenye kampeni tunashiriki kwa wingi na kusikiliza sera za wagombea,’amesema.
Halima Suleiman Ali mkazi wa Mtambile aliegombea Udiwani wadi ya Mtambile amesema uchaguzi wa mara hii umeonesha mwanga kwao, kwani wamewezeshwa kimafunzo, amekua na uthubutu na amejitokeza kwenye kinyn’ganyiro cha kuwania uongozi.
‘’Sijawahipo hata siku moja kuchukua fomu, ila Kutokana na ushirikishwaji kupitia mashirika na jumuiya mbalimbali mwaka huu nimethubutu kujitupa jimboni na kuusaka udiwani”
Kwa upande wake Amina Abdala Saidi mwenye ulemavu wa viungo mteule wa nafasi ya udiwani viti maalumu Chama cha ACT WAZALENDO Wadi ya Changaweni Mkoani, amesema uchaguzi wa mwaka huu baadhi ya mambo yamebadilika, na ndio maana akafanikiwa kupata nafasi hiyo.
Amesema katika chaguzi zilizopita hata baadhi ya vituo vya uchaguzi havikua na mazingira rafiki kwa mtu mwenye ulemavu,tunaamini uchaguzi huu mambo yatabadilika,’’alisema.
Maabadi Abdala mwenye uoni hafifu kutoka Sizini allishauuri kuwekwa mazingira rafiki, ambayo yatawawezesha kupata fursa ya kuwatilia kura viongozi wanaowataka, ili kuepuka kupigiwa na watu wengine, jambo ambalo linaweza kupelekea kutiliwa wasiowataka wenyewe.
Hidaya Mjaka Ali, mwanaharakati wa Jumuia ya Watu wenye ulemavu Zanzibar JUWAUZA amesema uchaguzi wa mwaka huu mambo yamebadilika, na kupelekea jumla ya wanawake wenye ulemavu 12 kujitokeza kuchukua fomu za kugombea, ambapo haijawahi kutokea.

Aidha amesema licha ya hilo bali wanaomba kuwekewa mazingira rafiki katika vituo vya kupiga kura,ili kila mwenye ulemavu apate haki yake ya kupiga kura.
Mashavu Juma Mabrouk kutoka Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Ofisi ya Pemba, amesema hali ya mwaka huu inaonyesha mabadiliko,licha kwamba bado kuna ukakasi.
‘’Katika chaguzi zote zilizopita mazingira hayakua rafiki kwa Wenye Ulemavu, tunaomba marahii wawekewe miundombinu wafike vituoni na kupiga kura,’’alisema.
Afisa Mfawadhi kutoka Tume ya Haki za Binadamu Ofisi ya Pemba Suleimana Salim Ahmad amesema kufuatia mabadiliko madogo juu ya ushiriki mzuri wa watu wenye ulemavu katika upigaji kura,ni vizuri Tume ya uchaguzi kuweka maringira rafiki kwa watu hao, wapate kupiga kura kama watu wengine, wasio na ulemavu.
Juma Msanif Sheha Mkuu wa Programu kwa wapiga kurana msimamizi kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC amesema wamejipanga kuweka wakalimani, mashine ya nukta nundu na vitambulisho maalumu kwa watu wenye ulemavu katika vituo vya kupigia kura, ili kuwarahisishia kupata haki yao ya kikatiba ya upigaji kura.
Jumla ya watu 7891 Wenye Ulemavu wanatarajia kupiga kura katika uchaguzi mwaka huu.
Chama cha wandishi wa Habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar TAMWA- ZNZ kimekua kikichukua hatua mbali mbali, kuona wanawake wenyeulemavu wanapewa nafasi sawa, mafunzo na katika michakato ya kampeni na uchaguzi.
Zanzibar ina Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.8 ya mwaka 2022, kifungu cha 20 kineleza umuhimu wa Watu Wenye Ulemavu kuweza kufikia miundombinu mbalimbali, pamoja na taarifa, mawasiliano na haki zote za kibinadamu na za msingi.
Aidha, Tanzania imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD), unaohimiza serikali kuhakikisha ushiriki sawa wa watu wenye ulemavu katika siasa na maamuzi.
Hata Katiba ya Zanzibar ya 1984, kupitia kifungu chake cha 21(1) nacho kinatambua haki ya kila raia kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi bila ubaguzi.





















