Na Siti Ali, Novemba 24, 2025.
Afisa Sheria Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Idrisa Khamis Daima, amesema kuwa kupitishwa kwa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu Barani Afrika kutaleta mafanikio makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuripoti na kusaidia watu wenye ulemavu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Tumekuja, Ndugu Idrisa alisema kuwa mkataba huo utakapokamilika utafungua ukurasa mpya wa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali ikiwemo kisiasa, kiuchumi na kijamii.
“Mkataba huu utawapa watu wenye ulemavu nafasi sawa katika kushiriki maamuzi ya kitaifa na kupata haki zao bila vikwazo. Ni hatua muhimu katika kujenga jamii jumuishi,” alisema.
Aidha, Afisa huyo amefafanua kuwa pamoja na manufaa makubwa yatakayopatikana kupitia mkataba huo, bado kuna changamoto kadhaa zinazoweza kujitokeza, ikiwemo tofauti za lugha, ambazo zinaweza kuathiri utekelezaji wa pamoja katika baadhi ya nchi za Afrika.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kikundi cha Utu cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Kusini, Ndugu Khayrun Khalid Mambo, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea waandishi uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuripoti kwa weledi masuala yanayowahusu watu wenye ulemavu.
“Waandishi wa habari ni daraja kati ya jamii na serikali. Tunahitaji kuripoti habari zenye kuhamasisha na kubadilisha mitazamo kuhusu watu wenye ulemavu,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yamelenga kuelezea maendeleo ya utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Binadamu na Watu Wenye Ulemavu Barani Afrika, na namna ambavyo Tanzania inachukua hatua kuunga mkono juhudi hizo za bara zima.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Bi. Marry Julias, ameeleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwakumbusha waandishi umuhimu wa kuripoti habari kwa mtazamo chanya unaolenga kusaidia watu wenye ulemavu na kuzitambua changamoto wanazokabiliana nazo kila siku.
“Tunataka kuona habari zinazowainua na kuwatetea watu wenye ulemavu, si zinazowaonyesha kama wategemezi. Habari zenu zinaweza kubadilisha maisha ya mtu,” alieleza.
Nao baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo walisema wamefarijika na elimu waliyoipata, wakiahidi kuifanyia kazi kwa vitendo kupitia kazi zao za kila siku.

“Tumepata uelewa mkubwa kuhusu haki na wajibu wetu katika kuripoti habari za watu wenye ulemavu. Tutaitumia elimu hii kuwafikia jamii na kuelimisha wengine,” alisema mmoja wa washiriki.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kuhakikisha vyombo vya habari vinakuwa mstari wa mbele katika kukuza usawa, ujumuishi na heshima kwa watu wenye ulemavu nchini.





















