Na Siti Ali. 21 July,2025
Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) imekutana na Ushirika wa Manahodha wa Mkokotoni Pangani kwa lengo la kusikiliza changamoto zao, kujadiliana kuhusu masuala ya usalama wa baharini na kuwapatia vifaa vya uokozi.
Akifungua kikao hicho cha siku moja, Mkurugenzi wa Ulinzi, Usalama na Mazingira ya Bahari wa ZMA, Kepteni Khamis Taji Khamis, amesema jukumu kuu la mamlaka hiyo ni kuhakikisha shughuli zote za usafiri baharini zinafanyika kwa usalama na kulinda mazingira ya bahari.
Kepteni Taji amewapongeza Manahodha hao kwa hatua ya kununua chombo maalum kwa ajili ya shughuli za uokozi baharini, akisema kitendo hicho kinaonesha uzalendo wa hali ya juu, na kuahidi kuwa ZMA itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha usalama unaimarika zaidi.

Kwa upande wake, Katibu wa Ushirika wa Manahodha wa Pangani Mkokotoni, Ahmada Haji Kombo (Gora), ameiomba ZMA kuanzisha kozi maalum za muda mfupi ili kuwaongezea ujuzi manahodha, akisema ni vigumu kwao kwenda Tanzania Bara kutokana na majukumu yao ya kila siku.
Baadhi ya manahodha waliopata nafasi ya kuzungumza, akiwemo Haji Ame Ameir wa Tumbatu Jongoe, Kombo Ali Kombo wa Tumbatu Kichangani, na Juma Jaku Kitiba, wamesema wananchi wengi wanaosafiri kati ya Mkokotoni na Tumbatu bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kuvaa life jacket.
Aidha walipendekeza ZMA kufanya ziara maalum ya kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa Tumbatu.

Naye Msimamizi wa ZMA Kanda ya Kaskazini Unguja, Simai Nyange Simai, amesema mamlaka kwa kushirikiana na manahodha hao imefanikisha usajili wa vyombo vya baharini, utoaji wa vitambulisho vya mabaharia, na uratibu wa shughuli za uokozi pale ajali zinapotokea.
Simai amepongeza uongozi wa manahodha kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwasisitiza kuendeleza ushirikiano wao kwa manufaa ya abiria na jamii kwa ujumla.
ZMA imekuwa na utaratibu wa kutembelea manahodha na mabaharia katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, kusikiliza changamoto zao, kuwapatia vifaa vya uokozi, na kutatua matatizo yao ili kuimarisha usalama na ulinzi wa abiria pamoja na mali zao baharini.





















