Home Uchumi Biashara ZANZIBAR YAANDIKA HISTORIA MPYA UWEKEZAJI UNAUFUATA SHERIA ZA KIISLAMU

ZANZIBAR YAANDIKA HISTORIA MPYA UWEKEZAJI UNAUFUATA SHERIA ZA KIISLAMU

26
0

Na siti Ali, 20 July, 2025.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mageuzi ya uchumi na fedha yaliyotekelezwa na Serikali yamekuwa nguzo muhimu katika kuijenga Zanzibar inayowashirikisha wananchi katika maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika hafla ya kumpongeza kwa mageuzi ya kiuchumi na kifedha pamoja na uzinduzi wa Skimu ya Hifadhi ya Jamii yenye kufuata misingi ya Kiislamu, iliyofanyika viwanja vya Ikulu Zanzibar, Dkt. Mwinyi alisema hatua hizo zimeweka msingi madhubuti wa kujenga uchumi shirikishi na imara.

“Mageuzi ya uchumi na fedha yaliyofanywa na Serikali yamekuwa msingi muhimu wa kuijenga Zanzibar inayowashirikisha wananchi katika ujenzi wa nchi,” alisema Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kutokana na sera madhubuti, mifumo ya kisasa na usimamizi bora wa fedha za umma, hali iliyochangia ukuaji wa uchumi kwa asilimia 7.2, ongezeko la uwekezaji wa ndani na nje, pamoja na udhibiti wa mfumuko wa bei kwa tarakimu moja.

“Tumeona ongezeko la mapato kwa asilimia 278 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, sambamba na kuimarika kwa sekta kama utalii, kilimo na uvuvi,” alifafanua Rais Mwinyi.

Aidha, amebainisha kuwa mageuzi hayo yamefanyika chini ya misingi ya uwazi, uwajibikaji na matumizi bora ya teknolojia za kisasa, hatua inayoongeza imani ya wananchi na wawekezaji katika mifumo ya Serikali.

Kuhusu mafanikio ya mfumo wa Zanzibar Sukuk, Rais Mwinyi alisema Serikali imeanza kutoa gawio la kwanza kwa wawekezaji kufuatia kuanzishwa kwake mwaka 2024, hatua inayoonyesha dhamira ya Serikali kusimamia kwa ufanisi dhamana zake.

“Kupitia Sukuk, Serikali imeweza kugharamia miradi ya kimkakati na kuimarisha imani ya wawekezaji, huku ikifungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya nchi,” alisema.

Akizungumzia historia ya mageuzi hayo, Rais Mwinyi alisema Zanzibar sasa inaingia katika hatua mpya ya kifedha inayofuata sheria za Kiislamu, jambo linaloongeza chaguo kwa wawekezaji na wananchi wanaofuata misingi hiyo.

“Hatua hii inaiweka Zanzibar katika historia mpya ya kifedha inayohusiana na uwekezaji unaofuata sheria za Kiislamu,” alisema

Rais Mwinyi.

Aliongeza kuwa Serikali imeanzisha mfumo wa bima wa Kiislamu kupitia Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), utakaotoa huduma za bima kwa misingi ya sheria za Kiislamu.

“Mafanikio ya uchumi shirikishi hayawezi kupatikana bila kuwepo mfumo imara wa bima, hivyo Serikali imeanzisha mfumo wa bima wa Kiislamu utakaotoa huduma kwa misingi ya sheria hizo,” aliongeza.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Mwinyi alisema mageuzi makubwa yamefanyika katika mifumo ya hifadhi ya jamii ili kuimarisha utendaji na kuhakikisha michango na malipo ya wastaafu yanasimamiwa kwa uwazi na ufanisi.

“Serikali imefanya mageuzi makubwa katika mifumo ya hifadhi ya jamii kwa kuimarisha utendaji na kuhakikisha michango inasimamiwa kwa uwazi, na faida zinawanufaisha wanachama,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa kupitia mifumo ya kidijitali, Serikali itahakikisha kila mfanyakazi anasajiliwa kwa ajili ya ulinzi dhidi ya changamoto za kiuchumi, uzee na maradhi, hatua ambayo itaijenga Zanzibar yenye haki na ustawi wa jamii.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Mhe. Saada Mkuya Salum, alimkabidhi Rais Dkt. Mwinyi tuzo maalum kutambua mchango wake katika mageuzi ya uchumi na sekta ya fedha nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here