Na Siti Ali.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye ubora ni nguzo muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo na utungaji wa sera bora nchini.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil, Kikwajuni, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi, amesema kuwa takwimu bora husaidia serikali kufahamu mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, na kuwezesha uundaji wa sera imara zenye tija kwa taifa.
“Kuwepo kwa takwimu bora na sahihi kutaisaidia serikali kuunda sera zenye msingi wa ukweli, kuelewa mabadiliko ya dunia, na kuchangia katika maendeleo endelevu ya nchi,” amesema Mwinyi.
Aidha, Mwinyi alizitaka taasisi zote za serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha zinashirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu, ili kuhakikisha taarifa zinazotumika kwenye mipango ya maendeleo zinakuwa na ubora na uhalisia unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ndugu Salum Kassim Ali, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu, ikiwemo kutumia teknolojia za kisasa katika ukusanyaji, uchambuzi na uhifadhi wa taarifa.
Amefafanua kuwa Serikali tayari imeandaa Dira ya Maendeleo ya 2050, ambayo inalenga kuifanya Zanzibar kufikia uchumi wa kipato cha juu kupitia maendeleo endelevu na jumuishi kwa watu wote, na kwamba utekelezaji wa dira hiyo unategemea takwimu bora zitakazosaidia kupima mafanikio na kuelewa mwenendo wa maendeleo katika sekta mbalimbali.

“OCGS itaendelea kutoa takwimu sahihi, za wakati na zenye viwango vinavyokubalika kimataifa, ili kusaidia serikali, sekta binafsi, wanahabari, na wadau wengine kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi,” alisema Ali.
Ameongeza kuwa takwimu ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo ya kimataifa kama vile Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs 2030), pamoja na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, ambazo zote zinahitaji taarifa sahihi za kufuatilia utekelezaji wa malengo ya kijamii, kiuchumi na mazingira.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na watumishi wa serikali, wadau wa sekta binafsi, wanafunzi na wanazuoni kutoka taasisi mbalimbali, ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili umuhimu wa matumizi ya takwimu katika nyanja za afya, elimu, uchumi na kilimo.

Kila ifikapo tarehe 20 Oktoba, na kila baada ya miaka mitano, Umoja wa Mataifa huadhimisha Siku ya Takwimu Duniani, ikiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya takwimu bora katika kupanga na kutathmini maendeleo ya jamii.
Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: “Kuchochea Mabadiliko Kupitia Takwimu Bora na Taarifa kwa Watu Wote.





















