Na Siti Ali.
Askari Polisi nchini wametakiwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika kubaini, kuzuia na kutanzua makosa yanayotokana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ili kukomesha vitendo hivyo na kuhakikisha jamii inabaki kuwa salama.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mkuu wa Polisi Jamii Zanzibar, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jonas Mahanga, amesema hayo katika Chuo cha Polisi Zanzibar wakati wa mafunzo ya Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kuhusu utendaji wa Madawati ya Jinsia.

Amesema kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji, bado matukio hayo yanaendelea kujitokeza kwa uchache katika baadhi ya maeneo, hivyo amewataka watendaji wa Madawati ya Jinsia kuendelea kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia Makao Makuu ya Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faidha Suleiman, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa utendaji Maafisa, Wakaguzi na Askari katika kubaini, kuzuia na kukabiliana na makosa ya udhalilishaji, na hatimaye kupunguza makosa hayo katika jamii.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mikakati inayoendelea ya Jeshi la Polisi kuhakikisha Dawati la Jinsia linafanya kazi kwa ufanisi katika kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji nchini.





















