Na Mwandishi wetu Pemba.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Hawah Ibrahim Mbaye, amezitaka taasisi za umma na binafsi kuhakikisha zinaandaa na kusimamia sera bora za matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na wadau wa taasisi mbalimbali za umma katika mkutano wa uchanganuzi wa mazingira ya udhibiti wa TEHAMA uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema ni wakati sasa kwa taasisi zote kujipanga kutumia teknolojia kwa ufanisi zaidi.
“Serikali inasisitiza kila taasisi kuwa na sera madhubuti ya matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati, kwa ufanisi na kwa uwazi. Dunia inabadilika, na taasisi zetu hazipaswi kubaki nyuma,” alisema Hawah Ibrahim Mbaye.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kidigital Tanzania (PC-DTP), Bakari Mwamgugu, alisema mradi huo unalenga kuleta mapinduzi chanya katika sekta ya TEHAMA kwa kuhakikisha taasisi za serikali na binafsi zinatumia teknolojia kuboresha mfumo wa kazi na mawasiliano.
“Tunataka kuona taasisi zote zinanufaika na maendeleo ya teknolojia, hasa katika ukusanyaji wa taarifa, utoaji huduma kwa wananchi na kuboresha utendaji wa ndani,” alieleza Mwamgugu.

Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo wamesema utekelezaji mzuri wa sera za TEHAMA utasaidia kuongeza uwazi, kurahisisha majukumu ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“TEHAMA imerahisisha kazi nyingi. Ikiwekwa vizuri, itasaidia sana katika kupunguza urasimu na kuongeza uwajibikaji serikalini,” alisema Ali Hassan, mmoja wa washiriki wa mkutano huo.
Mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kujadili mazingira bora ya udhibiti wa TEHAMA visiwani Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanakwenda sambamba na sera za kitaifa za kidigitali.





















