Home Jamii WAANDISHI VIJANA ZANZIBAR WANOLEWA KUTAMBUA TAARIFA SAHIHI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

WAANDISHI VIJANA ZANZIBAR WANOLEWA KUTAMBUA TAARIFA SAHIHI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

34
0

Na Mwandishi wetu Zanzibar.

Waandishi wa habari vijana visiwani Zanzibar wamepatiwa mafunzo maalum ya kutambua taarifa sahihi, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa lengo la kuwawezesha wanahabari vijana kujenga uwezo wa kuchambua, kuthibitisha na kuripoti taarifa zenye uhakika katika zama hizi za teknolojia ya kidijitali.

Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Kituo cha Huduma za Sheria kilichopo Kijangwani, Mjini Unguja, Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Simbaya, amewataka waandishi wa habari vijana kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya habari ili kuendana na kasi ya dunia ya sasa.

Simbaya amesisitiza umuhimu wa kujifunza na kutumia taaluma ya akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika kuhakiki taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha umma unapata habari zilizo sahihi na zenye vyanzo vya kuaminika.

“Katika dunia ya leo, taarifa nyingi zinazotolewa mitandaoni hazina uhakika. Ni wajibu wa mwandishi kutumia teknolojia na maarifa ya AI kuhakikisha habari anayoitoa ni sahihi na haina upotoshaji,” amesema Simbaya.

Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar, Abdallah Abdul Rahman Mfaume, amewataka washiriki kutumia maarifa waliyopata kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi.

“Waandishi vijana ndio nguvu mpya katika tasnia ya habari. Ni jukumu lenu kuhakikisha mnakuwa mstari wa mbele katika kutumia teknolojia na kutoa habari zenye ukweli, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi,” amesisitiza Mfaume.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru UTPC kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wamesema yamewaongezea uelewa juu ya teknolojia na mbinu za kisasa za ukusanyaji na uchambuzi wa habari

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na waandishi wa habari vijana kutoka Unguja na Pemba, na yamelenga kuwajengea uwezo wa kutambua taarifa sahihi na kupambana na upotoshaji wa habari katika majukwaa ya kidijitali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here