Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuwapa kipaumbele na kuwazingatia watu wenye ulemavu na wale wenye mahitaji maalum katika awamu yake ijayo ya uongozi.

Ahadi hizio amezitoa wakati alipokutana na kundi hilo katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibzr, ambako aliendelea na kampeni za kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi. ameeleza kuwa mapendekezo yanayowalenga watu wenye ulemavu ni pamoja na kuongeza uwakilishi wao katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi ikiwemo Baraza la Wawakilishi, kutekeleza Sera ya Uwezeshaji kwa ajili ya nafasi za uongozi, ajira na elimu, na kuweka mgao maalum wa fedha na mafunzo ya ujasiriamali.

Aidha, Dkt Mwinyi ameeleza dhamira ya Serikali ni kuhakikisha miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye ulemavu inajengwa katika masoko na majengo mapya, kuondoa ushuru kwa vifaa vya watu wenye ulemabu vinavyoingizwa nchini na kuendelea kuwapatia vifaa hivyo bila malipo. Hatua nyingine ni kuanzisha One Stop Center ya huduma za matibabu kwa watu wenye ulemavu, na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kuandaa utaratibu maalum wa ushiriki wao kwenye michezo.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa Serikali italifanyia kazi suala la ruzuku kwa vyama vya watu wenye ulemavu ili viweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.





















