Na: Samira Saidi.
Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, iliyorekebishwa na kuifanya Tanzania kuwa taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hii ni sehemu muhimu ya historia ya kisiasa ya nchi yetu, inayodhihirisha kuimarika kwa demokrasia kupitia ushiriki wa vyama mbalimbali katika uchaguzi, pamoja na kudumishwa kwa amani wakati wa mchakato huo.
Kupitia mfumo huu, wananchi wamepata fursa ya kugombea nafasi za uongozi katika ngazi tofauti, zikiwemo udiwani, uwakilishi, ubunge, na hata urais.
Mwenyekiti Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo na Vijana wa Chama cha Wakulima, Said Kheri Ame, kutoka Jimbo la Malindi, anaeleza namna demokrasia inavyotoa haki kwa kila mwananchi kugombea katika chama anachokipenda.
“Nchi yetu ya Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, kwa hiyo wakati wa uchaguzi kila mmoja ana haki ya kwenda kwenye chama chochote na kufanya maamuzi yake.”

Katibu mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan, ameeleza kuwa vijana wanapaswa kutumia nafasi waliyonayo kwa kuchukua hatua madhubuti katika kuleta mabadiliko chanya kupitia kura zao na michango yao katika jamii. Amesema ni wajibu wa kila kijana kuwa sehemu ya maamuzi yanayohusu mustakabali wao na taifa kwa ujumla.

“Natoa wito kwa vijana wote wa Tanzania kujitokeza na kushiriki kwa wingi siku ya Uchaguzi tarehe 29 Oktoba 2025 kwa kuhakikisha wanapiga kura ili kuchagua viongozi ambao watawaletea maendeleo na kuwa sauti ya vijana huku wakidumisha amani na usalama nchini,” amesema Ndugu Hassan.
Faiza Nassor ni afisa Programu wa pamoja youth Initiative yeye anaeleza kuwa lengo la mradi wa sauti yetu ni kuwawezesha vijana kushiriki katika uchaguzi michakato ya siasa na uongozi , pamoja na kuhamasisha ushiriki wa vijana katikangazi za maamuzi ambapo kwa wakati wa sasa idadi ya vijana ni ndogo.

Ushiriki wa Vijana Katika Mchakato wa Uchaguzi
Vijana ndio nguvu kazi kuu ya taifa, wakiwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya vijana 21,312,411 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35, sawa na asilimia 34.5 ya watu wote nchini. Kati yao, Tanzania Bara ina vijana 20,612,566 (sawa na 34.4%) huku Zanzibar ikiwa na vijana 699,845 (sawa na 37.0%) ya wakazi wake.
Ushiriki wa vijana katika michakato ya uchaguzi, ikiwemo kugombea nafasi mbalimbali na kupiga kura, ni hatua muhimu ya kudumisha demokrasia na kuchangia mabadiliko katika mifumo ya utawala.
Kuna mambo kadhaa ambayo vijana wanapaswa kuyazingatia ili kufikia malengo yao na ndoto zao, yakiwemo nidhamu, kujituma, kujifunza, ujasiri, na kufanya maamuzi sahihi. Vijana wengi nchini wamekuwa wakichukua hatua za makusudi kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa, uchaguzi na uongozi, kwa kutambua kuwa maamuzi hayo yanagusa na kuathiri maisha yao moja kwa moja.
Said Kheri Ame, ambaye ni mgombea wa ubunge wa Jimbo la Malindi kupitia Chama cha Wakulima (AFP), anaelezea kilichomsukuma kugombea katika uchaguzi.
“Nimeingia katika harakati hizi za kugombea ubunge kwa kuwa nina imani nina uwezo wa kuwatumikia wananchi wangu. Nimejiandaa kikamilifu na naamini nitashinda kutokana na sera zangu nzuri kwa wana Malindi.”
Sambamba na hilo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeeleza kuwa amilango iko wazi kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanaharakati, asasi za kiraia, na taasisi za vijana kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya uraia na uhamasishaji wa upigaji kura. Hatua hii inalenga kuongeza uelewa wa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu kuhusu haki zao za kidemokrasia na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi. Aidha Tume hiyo imesisitiza kuwa wadau wote wanatakiwa kufuata taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa njia sahihi na yenye kuzingatia misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Murugenzi wa Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano kwa Umma, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Juma Sanifu sheha katika uzinduzi wa Mradi wa Sauti yetu Unaotekelezwa na Pamoja Initiative, ameibainisha kuwa Tume ipo tayari kushirikiana na taasisi zote zenye nia njema ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa makundi mbalimbali katika uchaguzi.
“Milango iko wazi kwa asasi za kiraia zinazotaka kutoa elimu ya uraia kwa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu katika masuala ya kupiga kura, mradi tu zifuate taratibu zilizowekwa na Tume,” amesema Juma Sanifu.
Elimu ya Siasa na Uongozi kwa Vijana
Ili kuhakikisha vijana wanapata uelewa wa kutosha kuhusu siasa na uongozi, miradi mbalimbali imekuwa ikiwaandaa na kuwajengea uwezo kuwa viongozi bora wa kesho. Vyama vya siasa navyo vimekuwa vikitumia fursa hiyo kutoa mafunzo ya siasa na ugombea, ili vijana wawe na weledi na uthabiti wa kushiriki katika siasa kwa ujasiri.
Mgombea wa Chama cha Wakulima (AFP) Said Kheri Ame anaeleza kuwa Amesoma kozi mbalimbali zikiwemo ujasiriamali, sayansi ya siasa, maendeleo ya vijana na elimu ya uchaguzi. Baadaye alipewa mafunzo kutoka vyuo tofauti vilivyomuwezesha zaidi katika uongozi.
“Nimesoma kozi mbalimbali zikiwemo ujasiriamali, sayansi ya siasa, maendeleo ya vijana na elimu ya uchaguzi. Baadaye nilipata mafunzo kutoka vyuo tofauti vilivyoniandaa zaidi kwa uongozi.” Ameeongeza said.
Miradi Inayowawezesha Vijana Kushiriki Kidemokrasia
Miradi kama “Sauti Yetu” inayoendeshwa na Pamoja Youth Initiative (PYI), imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha vijana wa Zanzibar kushiriki katika michakato ya kidemokrasia na uchaguzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Pamoja Youth Initiative (PYI), Rashid Mwinyi amesema Lengo la mradi huo ni kuhakikisha sauti ya vijana inasikika katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuongozi na kijamii.

Sera za Mgombea wa Ubunge wa Malindi
Katika kampeni zake, Said Kheri Ame ameahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Malindi.
“Wana Malindi, nawaahidi maendeleo na mageuzi chanya. Malengo yangu makubwa ni kutatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kujenga chuo cha amali kitakachotoa mafunzo ya ujasiriamali, ushonaji na stadi mbalimbali. Pia nitawawezesha vijana kwa kuwatafutia mashamba ya kulima ili wapate kipato cha uhakika,” ameeleza.
Mbali na shughuli za kisiasa, Said Kheri Ame ni mwalimu wa sayansi, mwandishi wa habari, na mkurugenzi wa vyuo vya amali, ikiwemo Chuo cha Green Women kilichopo Miembeni, Zanzibar.
Wasifu Wake wa Elimu
Akielezea kuhusu wasifu wake wa elimu, Said Kheri Ame ameanza masomo yake ya msingi katika skuli za Muembe Ladu, Mfeneseni na Mkunazini. Baada ya hapo alichukua mchepuo wa sayansi katika Shule ya Sekondari ya Lumumba hadi kidato cha sita, na baadaye alihitimu elimu ya juu katika vyuo mbalimbali akiwa na Diploma ya Ualimu wa Sayansi (SUZA) na Uandishi wa Habari.
Katika kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kuwa vviongozi Said Kheri Ame amewaomba wananchi kuwatumia vijana kama chachu ya maendeleo katika taifa.
“Wito wangu kwa jamii ni kuwachagua vijana, Nguvu kazi ya taifa ni kijana, na kijana akikuahidi kitu anaweza kutekeleza.”
Wiki ya vijana mwaka huu , inaadhimishwa kuanzia tarehe 8 hadi Oktoba 14 Jijini Mbeya , ikitambua mchango wao katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.





















