Na mwandishi wetu.
Baraza la Vijana Zanzibar (BVZ) limesema litaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za vijana ndani na nje ya nchi katika juhudi za kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ndugu Ali Haji Hassan, wakati wa shughuli ya kufanya usafi na upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Kitengo cha Wazazi (META), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayoendelea kufanyika mkoani Mbeya.

Hassan amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinapojitokeza, vijana, wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa, hivyo ni muhimu vijana kuungana na kuunga mkono jitihada za serikali zote mbili katika kulinda mazingira.
“Jukumu la kutunza mazingira, kuifanya Tanzania kuwa ya kijani, na kupanda miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni letu sote, hasa sisi vijana,” amesisitiza Katibu Mtendaji huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Empower Youth Prosperity (EYP), Ipyana Mwakyusa, aliipongeza Baraza la Vijana Zanzibar kwa jitihada zao za kushirikiana na taasisi nyingine katika shughuli za maendeleo ya vijana wakati wa Wiki ya Vijana.

“Natoa wito wa kuendelea na mashirikiano zaidi katika masuala ya mazingira. Tunaahidi kuwa wasimamizi wazuri wa miti tuliyopanda leo na kuhakikisha inakua na kuwa kivutio kwa wageni wa hospitali hii,” alisema Mwakyusa.
Naye Afisa Afya wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Julieth George, aliwashukuru vijana kwa kuichagua hospitali hiyo kuwa sehemu ya zoezi hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya shughuli hizo kuwa endelevu na siyo kwa matukio maalum pekee.
Shughuli hiyo imefanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Vijana Zanzibar (BVZ), Empower Youth Prosperity (EYP), na wadau wengine wa maendeleo ya vijana waliopo Mbeya. Mradi huo unatekelezwa chini ya mpango wa Vijana Plus unaoratibiwa na Save the Children kwa kushirikiana na Tanzania Bora Initiatives (TBI), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).





















