Na Siti Ali,
Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani, Ndugu Hemed Suleiman Abdulla, amesema akichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo anawaahidi kuwawezesha wajasiriamali na vikundi vya ushirika ili kukuza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika muendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi maalum katika vijiji vya Mchakwe na Jombe kwa Sanani, amesema dhamira yake ni kuona vijana na wanawake wa Jimbo la Kiwani wanapata mitaji, mikopo isiyo na riba, pamoja na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi zao.

Ameeleza kuwa atahakikisha wajasiriamali wanapatiwa elimu ya biashara na soko la uhakika, jambo litakalosaidia kukuza kipato na kuleta maendeleo endelevu jimboni humo.
Kuhusu sekta ya michezo, Hemed ameahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na wanamichezo kwa kuwapatia vifaa vya mazoezi na kuwaletea wakufunzi watakaowajengea uwezo wa kufanya mazoezi kwa njia bora na salama.
Aidha, katika sekta ya elimu, ameahidi kwamba kwa kushirikiana na viongozi wenzake watajenga skuli kubwa ya kisasa katika kijiji cha Mchakwe ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Hemed ameongeza kuwa miundombinu ya barabara imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo jimboni humo, na kwa kutambua hilo, atahakikisha barabara ya Mchakwe–Branji inajengwa ili kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi.
Amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia nafasi serikalini na katika sekta binafsi, sambamba na kuwawezesha kujiajiri kwa kuwapatia nyenzo na maarifa.

Vilevile, ameahidi kuimarisha ulinzi shirikishi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa Polisi Jamii na kuhakikisha wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi wanapatiwa pensheni jamii kwa wakati.
Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na umoja, akisema bila ya amani hakuna maendeleo yanayoweza kufikiwa.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Kiwani, Ndugu Hija Hassan Hija, amesema akichaguliwa kuwa mbunge ataimarisha huduma za afya kwa kuhakikisha wananchi wanapata matibabu na vipimo bure, huku mama wajawazito wakijifungulia ndani ya jimbo hilo bila gharama.
Ameongeza kuwa watakapopata ridhaa ya uongozi, watahakikisha wazazi hawachangii gharama za masomo katika skuli na madrasa, kwani serikali itachukua jukumu hilo kama sehemu ya kuboresha elimu.

Naye Mgombea Udiwani wa Wadi ya Mwambe, Ndugu Nassor Bakari, amesema Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM kwa kujenga miradi ya maendeleo ikiwemo skuli za kisasa, barabara na huduma za kijamii zinazowanufaisha wananchi wa Jimbo la Kiwan.





















