Home Jamii KUJITOLEA NA MASHIRIKIANO NDIYO NJIA YA KUFANIKISHA MALENGO: ALI HAJI HASSAN

KUJITOLEA NA MASHIRIKIANO NDIYO NJIA YA KUFANIKISHA MALENGO: ALI HAJI HASSAN

28
0

Na: Siti Ali.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, amesisitiza umuhimu wa kujitoa kwa vijana ili kujenga mitandao ya ushirikiano na kuonyesha taswira bora kwa vijana wenye maono, hatua inayowawezesha kufanikisha ndoto zao.

Akizungumza katika kikao cha kujenga mashirikiano kati ya Baraza la Vijana Zanzibar na Taasisi ya Empower Youth Prosperity (E.Y.P) ya Jijini Mbeya, katika ofisi za Taasisi hiyo, Ali Haji Hassan amesema kuwa vijana wengi wanashindwa kufanikisha malengo yao kutokana na ukosefu wa moyo wa kujitolea katika harakati za kila siku.

Akitaja umuhimu wa mitandao ya kijamii, amewataka vijana kuitumia vyema ili kujijitangaza, kutangaza shughuli wanazozifanya, na kutafuta fursa zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi badala ya kusubiri ajira za Serikali pekee.

Akielezea utendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, amesema kuwa baraza hilo ni chombo kinachowakilisha maslahi ya vijana ndani na nje ya nchi, ambapo mabaraza madogo yanapatikana ngazi za Shehia, Wilaya, na Taifa, na kuunganisha vijana katika harakati za maendeleo ya kijamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Empower Youth Prosperity (E.Y.P), Ipyana Mwakyusa, ameeleza kuridhishwa na ugeni huo na kuwaomba taasisi na wadau wa maendeleo ya vijana kutambua kuwa Taasisi hiyo ni sehemu muhimu ya kubadilisha mitazamo, kujenga umoja, na kuchochea mabadiliko chanya kwa jamii.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya vijana yatafikiwa kupitia ushirikiano wa pamoja kati ya vijana, Serikali, na wadau wa maendeleo ya vijana, jambo linaloweza kuleta mabadiliko chanya na endelevu kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here