Home Jamii ACT WAZALENDO YAZINDUA ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2025, YAAHIDI MAGEUZI MAKUBWA ZANZIBAR

ACT WAZALENDO YAZINDUA ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2025, YAAHIDI MAGEUZI MAKUBWA ZANZIBAR

28
0

Na Siti Ali, Zanzibar.

 Chama ACT Wazalendo kinalenga kufanya mageuzi makubwa katika nyanja za utawala, uchumi, elimu, afya na ustawi wa jamii, ili kujenga Zanzibar yenye haki, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Oktoba 8, 2025, katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Ilani hiyo imebeba matumaini mapya kwa Wazanzibari, ikilenga kurejesha thamani ya utu, haki na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wote.

“Tumekutana hapa tukiwa tumebaki na siku chache kabla ya Wazanzibari hawajachagua hatima yao. Ilani hii ni zao la fikra za pamoja na vilio vya wengi wanaotaka mwelekeo mpya wa Zanzibar,” amesema Mhe. Othman.

Aidha Mhe Othman ametaja misingi minne mikuu ya Ilani hiyo kuwa ni Uchumi, Mamlaka, Haki, na Jamii ambapo, Chama hicho kinapendekeza kuchochea uchumi kupitia kilimo na uvuvi wa kisasa, utalii wa staha na ujasiriamali, kuimarisha mamlaka ya Zanzibar ndani ya Muungano, kupambana na rushwa na ufisadi,  na kurejesha utengemano wa kijamii kupitia maridhiano na malezi bora ya watoto.

Sambamba na hayo, amevitaja vipaumbele vitano vikuu vya ACT Wazalendo katika kipindi cha miaka ijayo vitakuwa ni Mamlaka ya Zanzibar na Utawala – kupitia mkataba wa Muungano na mabadiliko ya katiba, Utengemano wa Kijamii na Utamaduni kwa kuimarisha maridhiano na maadili ya kitaifa, Uwajibikaji na Utawala wa Sheria ambayo ni mageuzi katika mifumo ya haki na uchaguzi. Jamii na Uchumi Shirikishi ambayo ni mageuzi ya kikodi, pensheni na hifadhi ya jamii, pamoja na Teknolojia na Maendeleo Endelevu yakilenga kukuza sekta ya mawasiliano, utafiti na ubunifu.

ilani hiyo imzinduliwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, utakao husisha uchaguzi wa urais, ubunge uwakilishi na udiwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here